Na Mwandishi wetu, Dodoma
Jamii imetakiwa kujenga tabia ya kujitegemea na kufanya kazi ili kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 22, jijini Dodoma na Rais wa Chama cha wataalamu wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) Wambura Sunday wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ikiwa ni kuelekea Mkutano Mkuu wa nne wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nchini.
Sunday amesema nchi ya Tanzania imejengwa katika misingi ya kujitegemea hivyo watalaamu wa maendeleo ya Jamii wana wajibu wa kuwafikia wananchi na kuwasisitiza kuendeleza dhana hiyo.
“Tunalenga maisha ya kujitegemea, tunataka jamii ya Tanzania iweze kujitegemea katika maisha yao ya kila siku,” amesema Wambura.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Paschal Mahinyila amewahimiza wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kutimiza majukumu yao wa weledi.
Amesema kupitia Chama hicho, tayari rasimu ya muongozo wa maadili, miiko na viwango vya Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii umeandaliwa.
Naye Mratibu wa Chama hicho kanda ya Ziwa, Aliadina Peter, amesisitiza. kuwa katika Mkutano Mkuu huo, wanachama wajadili changamoto na kuzitatua kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.
Mkutano huo utakaofanyika kuanzia Februari 23, 2021 jijini Dodoma, utawahusisha Wadau wa Maendeleo ya Jamii zaidi ya mia nne kutoka nchi nzima.
Kauli mbiu ya Mkutano mwaka huu ni “Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ni nguzo muhimu ya kujenga jamii yenye kujitegemea jatika kuimarisha uchumi wa kati”.