24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yahimizwa kula vyakula vya asili

Na Allan Vicent, Tabora

MAADHIMISHO ya Siku ya Lishe Duniani yanayofanyika Kitaifa mkoani Tabora yamezinduliwa jana na Mkuu wa Mkoa huo Dk. Batilda Burian katika uwanja wa Nane Nane uliopo eneo la Ipuli mkoni humo huku mapishi ya vyakula vya asili yakiwa kivutio kikubwa.

Akizindua maonesho hayo Dk, Burian ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili kwa kuwa vina virutubisho vya lishe bora ambavyo vitasaidia sana kuimarisha afya zao.

Amesisitiza kuwa elimu ya lishe ni muhimu sana kwa kuwa itasaidia  jamii kutambua umuhimu wa kula vyakula vyenye virutubisho vya kutosha na kuacha kupika chakula kwa mazoea.

Alibainisha kuwa lishe bora inapaswa kuwa agenda ya kudumu na kuhubiriwa katika mikutano yote inayofanyika katika halmashauri za Mkoa huo ili kupunguza matatizo yatokanayo na lishe duni.

Ameongweza kuwa ulaji vyakula visivyo na lishe huchangia kwa kiasi kikubwa tatizo la udumavu kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5 na kwa akinamama wajawazito kujifungua watoto wasio na afya njema.

“Wakuu wa wilaya na Wataalamu wa halmashauri hamasisheni jamii kutumia vyakula vya asili kwa kuwa vina virutubisho vya lishe bora ambavyo vitawapa afya njema na nguvu za kufanya kazi,” amesema Dk. Burian.

Alionya kuwa kama jamii haitahamasishwa vya kutosha, kizazi kijacho kitaendelea kuathirika kwa kuwa hakitakuwa na nguvu za kutosha kufanya kazi, alishauri elimu itolewe katika vijiji na kata zote.

Aliwapongeza akinamama wa Mkoa huo kwa kuandaa vyakula vya asili ili kuonesha uhalisia wa vyakula vyenye virutubisho vya lishe ambavyo vimeungwa karanga, nazi na viungo vinginevyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tabora Dk. Yahaya Nawanda alimhakikishia RC kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyowapa ikiwemo kuhamasisha jamii kutumia lishe yenye virutubisho kamili.

Aidha Wakuu wa Wilaya, Paul Chacha (Kaliua), Kisare Makori (Uyui) na Luis Bura (Sikonge) walisema kuwa tayari wameanza kuhamasisha shule zote kuwapa chakula wanafunzi wao ikiwemo uji wenye lishe asubuhi.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Mkoani humo Said Ntahondi aliitaka jamii kupunguza ulaji wa vyakula vilivyoungwa na mafuta bali watumie vyakula lishe vilivyoungwa na viungo vingine.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufikia kilele chake kesho Jumamosi Oktoba 23, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Doroth Gwajima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles