26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

JAMHURI YAANZA KUTOA USHAHIDI DHIDI YA MANJI

PATRICIA KIMELEMETA NA SHABANI CHUWAKA

MASHAHIDI wawili wa upande wa Jamhuri, wameanza kutoa ushahidi wao katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili  mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji.

Mashahidi hao walitoa ushahidi wao jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mfawidhi Cyprian Mkeha, wakati walipoongozwa na wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis wakati Manji akitetewa na Wakili Hudson Ndusyepo.

Mashahidi hao, ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka Ofisi ya Mkuu wa  Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ramadhan Kingai(42) ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa watuhumiwa wa dawa za kulevya waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na askari wa upelelezi kutoka kanda hiyo, E 1125  Koplo Sospeter(49).

Kingai, alidai Februari 9, mwaka huu, alipokea watu wawili waliotajwa kwenye orodha ya mkuu wa huyo ambao wanadaiwa kujihusisha na utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

Alidai, watu hao ni  Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambapo aliwahoji na kuwapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili waweze kupimwa sampuli ya mkojo ili kuthibitisha kama kweli wanatumia au laa

Alidai  baada ya kupelekwa kwa mkemia, ripoti ya uchunguzi wa sampuli hiyo ilionyesha kuwa mfanyabiashara Yusuph Manji mkojo wake umekutwa na dawa za kulevya aina ya benzodiazepine, huku majibu ya mkojo wa askofu Gwajima ikionyesha hatumii dawa za kulevya.

“Mara baada ya kupimwa, mkemia alirudisha majibu ambayo yalionyesha kuwa, mkojo wa Manji umekutwa na dawa za kulevya aina ya benzodiazepine wakati majibu ya Gwajima alionyesha hatumii dawa za kulevya,”alidai kingai.

Alidai baada ya kupokea ,majibu hayo, ofisi hiyo ilimwachia Askofu Gwajima  wakati Manji alipelekwa mahabusu kwa ajili ya kusubiri jalada lake kupelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP), ili aweze kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Alidai kwa sababu kosa alilokutwa nalo ni la utumiaji wa dawa za kulevya, jambo ambalo liliifanya ofisi hiyo kumwandikia mashtaka.

Alidai, kwa sababu yeye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, alilazimika kutuma askari kwenda nyumbani kwa Manji kwa ajili ya kumkagua kama wanaweza kukuta makosa mengine, ambapo askari waliporudi walidai wamekuta vitu ambavyo havihusiani na makosa hayo.

Shahidi wa pili katika kesi hiyo ambaye ni koplo Sospeter alieleza mahakama hiyo kuwa, alipewa oda ya kumpeleka Manji kwa mkemia Mkuu ili aweze kuchukuliwa sampuli ya mkojo.

Alidai, wakati anapewa oda hiyo alipewa na fomu namba 0 1 ya sheria namba 5,2015 ya kuwasilisha sampuli ya mkojo kwa mkemia mkuu.

Alidai ilipojibiwa alipewa fomu nyingine pamoja na kichupa cha kuhifadhi mkojo ambacho walimkabidhi Manji ambacho kiliingizwa mkojo uliopelekwa kwa mkemia mkuu kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo.

“Mara baada ya kupewa oda ya kumpeleka Manji kupimwa mkojo nilipewa kichupa na fomu ya kujaza ambayo niliisaini, nilipofika kwa mkemia, walimpima na kunipa majibu ambayo yalionyesha anatumia dawa za kulevya.

“Majibu hayo niliyapeleka kwa afande Kingai ili aweze kuendelea na taratibu nyingine kwa sababu mimi kazi yangu ilikua imekwisha,”alieleza mahakama hiyo.

Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kuendelea na mashahidi wengine wawili wa upande wa jamhuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles