24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jamhuri imesema uongo kuhusu polisi – Profesa Lipumba

LipumbaNa Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema Jamhuri inasema uongo kwamba Jeshi la Polisi liliwanyima kibali cha kuandamana na kwamba akiwa na msafara wa magari alifuatana na wafuasi wake kuelekea Mbagala Zakhem.
Profesa Lipumba anadai si kweli kwamba walifanya maandamano, ispokuwa walipigwa tu wao na wala hawakukamatwa wakiwa katika maandamano.
Alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati mshtakiwa huyo na wenzake 31 walipokuwa wakisomewa maelezo ya awali ya kesi inayowakabili.
“Si kweli kwamba tulifanya maandamano, tulipigwa tu hatukuandamana sisi, wala hatukukamatwa katika maandamano,”alidai Profesa Lipumba.
Kwa kuongozwa na wakili wa utetezi, Twaha Taslima, walikana Januari 26, mwaka huu kunyimwa kibali cha kufanya maandamano kwa sababu hawakuwahi kuomba kibali, walitoa taarifa ya kufanya maandamano.
“Si sahihi kusema Polisi iliwanyima kibali, hapakuwa na maombi ya kibali, CUF walitoa taarifa ya kufanya maandamano,” alidai Taslima.
Pia Profesa Lipumba na washtakiwa wengine walikana kusikia Polisi wakitoa onyo katika maeneo ya ofisi za chama hicho wilayani Temeke wakiwataarifu waandamanaji kutawanyika kwani mkusanyiko haukuwa halali.
Washtakiwa hao walidai hawakuwa wakifahamiana, wote walikutana katika kesi na hawakuwahi kukaidi amri ya Polisi iliyowahi kutolewa ikiwazuia kufanya maaandamano.
Akiendelea kusoma maelezo hayo Wakili wa Serikali, Mohammed Salum, alidai washtakiwa wakiwa katika mzunguko wa eneo la Mtoni Mtongani walikutana na Polisi ambao walitoa onyo wasiendelee na maandamano.
Washtakiwa wote walikana kupokea onyo hilo na kuendelea kusisitiza kwamba hawakuwahi kufanya maanadamano.
Washtakiwa walikubali kwamba walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Januari 28 na 29 mwaka huu na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Profesa Lipumba alikubali kwamba kulikuwa na barua ya kulifahamisha Jeshi la Polisi kwamba kutakuwa na maandamano Januari 27 mwaka huu kuelekea katika Viwanja vya Mbagala Zakhem.
Alikubali Januari 27 mwaka huu alifika katika ofisi za chama hicho Temeke na kufanya mkutano mfupi na viongozi wilayani humo.
Baada ya kumaliza kusomewa maelezo hayo ya awali Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 4 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles