25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Jalada la kina Mbowe larejeshwa Kisutu

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru jalada la kesi ya vigogo wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe, waliokata rufaa kupinga kutiwa hatiani na adhabu lirejeshwe Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kukusanya mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa jana mbele ya Jaji Ilvin Mgeta baada mlalamikiwa Jamhuri kudai kwamba wamepokea mwenendo wa kesi, lakini kuna nyaraka zingine hazipo.

Akiwawakilisha warufani, Wakili Peter Kibatala alidai kuwa walalamikaji watano; Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu, Visiwani Zanzibar, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu John Mnyika na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche walikuwepo mahakamani.

Kibatala alidai kuwa walalamikaji, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Halima Mdee (Kawe) na Esther Bulaya (Bunda) wameshindwa kufika mahakamani kwa sababu ya matatizo ya afya zao.

Alidai kuwa walalamikaji wameridhia rufani hiyo kuendelea kusikikizwa bila uwepo wao.

Upande wa wajibu rufani ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraji Nchimbi akisaidiana na Wakili wa Serikali Salimu Msemo, ulidai kuwa kuendelea kusikiliza rufani bila uwepo wa walalamikaji watatu hawana pingamizi, wanaiachia mahakama.

Hoja ya walalamikiwa inajikita kwamba nyaraka walizopatiwa na Mahakama Kuu haziko sawa, zina kasoro ili waweze kuitetea rufani ya walalamikiwa dhidi yao.

Nchimbi alidai kuwa hatua za usikilizwaji zilipitia mahakimu wawili tofauti na zilitakiwa kuwa na kurasa kati ya 566 au zaidi.

Akijibu hoja za walalamikiwa, Kibatala alidai kuwa mawakili wote walishiriki kesi hiyo tangu inaanza mbele ya Jaji Wilbard Mashauri (wakati huo akiwa hakimu).

Alidai kuwa wao ni maofisa wa mahakama na Aprili 28, mwaka huu Jaji Mfawidhi, Lameck Mlacha rufani hiyo ilipotajwa mbele yake aliwauliza kama kuna lolote lakini pande zote mbili zilieleza ziko tayari kuanza kusikiliza jana.

“Mei 11, mwaka huu nilipata barua kutoka kwa Jaji Mfawidhi akisistiza kwamba tufike mahakamani kwa ajili ya kusikiliza rufani hiyo. 

“Tunapinga maombi ya walalamikiwa ya kutaka ahirisho, mahakama iwe na ukali kusimamia amri zake, kama itaahirishwa iwe kwa muda mfupi ili tuendelee na kusikiliza rufani hii,” alidai Kibatala.

Jaji Mgeta alisema mahakama yake imepokea majibu ya barua ya Mei 11, mwaka huu kutoka kwa walalamikiwa, wakielezea kasoro zilizopo kwenye mwenendo wa kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu.

“Mfano hakuna mwenendo wa Februari 24, mwaka huu na kuendelea,” alisema Jaji Mgeta.

Akitoa uamuzi, alisema kama kuna mwenendo wa mahakama nyingine tofauti na Kisutu utengwe pembeni.

Alisema mahakama yake inaamuru jalada hilo kurejeshwa Mahakama ya Kisutu, ikakusanye mwenendo jana na leo, kuanzia kesi ilipoanza hadi mwisho wa hukumu yake.

“Naagiza jalada hili lirejeshwe Mahakama ya Kisutu leo na kesho (jana na leo) wakakusanye mwenendo tangu kesi ilipoanza mpaka ilipotolewa hukumu.

“Ijumaa Mei 15, mwaka huu jalada lirejeshwe hapa ili pande zote mbili mpate nakala za mwenendo huo, Jumatatu Mei 18, mwaka huu tukutane hapa saa tatu asubuhi kuanza kusikiliza,” alisema Jaji Mgeta.

Mbowe na wenzake wamekata rufani Mahakama Kuu kupinga hukumu ya kulipa faini ya jumla ya Sh milioni 320 au kwenda jela  miezi mitano kwa kila kosa.

Rufani hiyo iliyosajiliwa kwa namba 76 mwaka huu imewasilishwa na Kibatala ikiwa na sababu 14.

Kwa mujibu wa hati ya rufani, walalamikaji wanadai kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwatia hatiani Mbowe na wenzake kwa sababu haikuchambua ushahidi wa Jamhuri wakati wa kuandika hukumu hiyo.

Hoja nyingine, Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake haikuonyesha sababu zilizosababisha washtakiwa kutiwa hatiani.

“Upande wa Jamhuri ni jukumu lao kuthibitisha makosa bila kuacha shaka na kwamba si kazi ya mshtakiwa kujitetea,” ilieleza sehemu ya hoja za walalamikaji.

Hoja nyingine, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba hakutilia manani utetezi wa washtakiwa Matiko na Mnyika kwamba katika ushahidi wa Jamhuri hakuna ulipoeleza kama walikuwepo kwenye tukio.

Kwamba pia mahakama ilikosea kuwatia hatiani washtakiwa katika shtaka lililokuwa na mashtaka manne ndani yake ikiwamo kufanya maandamano, kusababisha kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwiline na askari polisi wawili kujeruhiwa.

Hoja nyingine ni kwamba mahakama ilipokea CD iliyoonyesha maandamano ya washtakiwa kinyume cha sheria na kwamba utaratibu wa kisheria haukufuatwa na kielelezo hicho kilipokewa kiholela.

Katika kesi ya msingi, Mbowe na viongozi wenzake walishtakiwa kwa mashtaka 12 ya uchochezi na moja la kula njama.

Mashtaka 12 yaliyowakabili, katika shtaka la kula njama, walidaiwa kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2017,  wakiwa Kinondoni Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani kwa kutenda kosa la jinai na kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Bulaya alikabiliwa na shtaka la kushawishi kutenda kosa la jinai ambapo alidaiwa Februari 16, mwaka huo, katika viwanja vya Buibui Kinondoni, Dar es Salaam alishawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Washtakiwa wote Februari 16, mwaka huo, wakiwa katika barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja kinyume cha sheria, waliendelea na mkusanyiko katika namna iliyowafanya watu waliokuwa kwenye eneo hilo waogope watakwenda kwenye uvunjifu wa amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles