AGOSTI 31, 2012 aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Jakaya Kikwete, alitoa hotuba ya aina yake ambayo iliitikisa Malawi na nchi nyinginezo jirani wa Taifa hilo na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Jambo lililowagusa wengi katika hotuba hiyo, ni pale alipozungumzia juu ya mpaka kati ya Tanzania na Malawi, ambao kwa miaka mingi kumekuwa na mgogoro wa chini kwa chini baina ya nchi hizo mbili juu ya wapi zinatengana katika Ziwa Nyasa.
Ni kutokana na kufahamu hilo, hasa baada ya Malawi kuanza kurusha ndege zao katika eneo la Ziwa Nyasa ambalo Watanzania tunaamini ni eneo letu, Kikwete aliona ni vema kuliweka sawa hilo.
Hebu tuone nini alichosema Kikwete katika hotuba yake hiyo siku hiyo;
Ndugu wananchi; Kila mwisho wa mwezi nimekuwa nazungumza na taifa kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa taifa letu na watu wake. Leo nina mambo mawili ya kuzungumza nanyi.
Lakini, kama ilivyo mazoea yetu hatuna budi kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wetu, kwa kutujalia baraka zake, za uhai na uzima na kutuwezesha kuwasiliana leo Agosti 31 mwaka 2012.
Ndugu Wananchi; Jambo la kwanza ninalotaka kuzungumzia leo ni zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza Agosti 26, 2012 ambalo linatarajiwa kumalizika Septemba Mosi, 2012.
Mtakumbuka kuwa Agosti 25, 2012 nilizungumza nanyi na kuwaomba mjitokeze kwa wingi na muwape ushirikiano unaostahili Makarani wa Sensa watakapopita majumbani mwenu kutekekeza wajibu wao. Tumebakiza siku moja kufikia kilele cha sehemu ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Napenda kuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu wote kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa. Mpaka sasa mwelekeo ni mzuri na ugumu ulioonekana kuwepo pale mwanzoni uliendelea kupungua siku hadi siku kadiri utekelezaji wa zoezi ulivyokuwa unaendelea. Kwa mwenendo huu nina matumaini makubwa kuwa sensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio mazuri.
Ndugu Wananchi; Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa wale wote ambao hawajahesabiwa wafanye hivyo. Naomba waitumie siku moja iliyosalia yaani kufanya hivyo.
Aidha, namuomba Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Serikali ya Muungano na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa kasoro zo zote zilizopo mahali po pote zinatafutiwa ufumbuzi ili mambo yakamilike bila upungufu wowote.
Ndugu Wananchi; Baada ya kazi ya Makarani wa Sensa kuhesabu watu kufikia kilele chake, Septemba 2, 2012, linaanza zoezi la kuwashughulikia wale ndugu zetu ambao watakuwa bado hawajahesabiwa.
Itakuwepo fursa ya siku saba kwa watu hao kuhesabiwa.
Watatakiwa wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa wenyeviti wao wa Serikali za Mitaa au Vijiji. Taarifa hizo zitafikishwa kwa Kamishna wa Sensa kwa ajili ya kujumuishwa. Baada ya muda huo kwisha, zoezi la kuhesabu watu litakuwa limefika mwisho.
Yule ambaye atakuwa hakutumia fursa hizo mbili atakuwa amekosa kuingizwa katika hesabu ya Watanzania ya mwaka 2012. Napenda kuwasihi ndugu zangu, Watanzania wenzangu kutumia siku ya kuhesabiwa na kama hapana budi basi tumia fursa ya kupeleka taarifa zako kwa Mwenyekiti wako wa Mtaa au Kijiji katika siku saba zinazofuatia siku hiyo ili nawe ujumuishwe.
Ndugu Wananchi; Baada ya kazi ya kuhesabu watu kwa namna zote mbili kufikia mwisho, itaanza kazi ya uchambuzi na kuunganisha takwimu na taarifa zilizokusanywa.
Kazi hiyo ni muhimu na ni kubwa hivyo inahitaji umakini na uangalifu wa hali ya juu sana, kwani ikikosewa zoezi zima la Sensa litaingia dosari. Nafarijika kuhakikishiwa na Viongozi wa Sensa na Wakuu wa Idara za Takwimu za Serikali zetu mbili, kwamba wanatambua ukweli huo na wajibu wao.
Wameniarifu kwamba kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa, matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi ya watu na jinsia zao yatatolewa mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa nyingine zitafuata baadaye. Narejea kuwasihi Watanzania wenzangu kuwapa nafasi wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi ili tupate matokeo yaliyo sahihi.
Ndugu Wananchi; Jambo la pili ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni kuhusu mpaka baina ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa. Kama mjuavyo, kwa miaka mingi nchi zetu mbili zinatofautiana kuhusu wapi hasa mpaka uwe.
Sisi, Tanzania, tunasema mpaka upo katikati ya ziwa wakati wenzetu wa Malawi wanasema upo kwenye ufukwe wa ziwa upande wa Tanzania. Kwa maneno mengine wanasema ziwa lote ni mali ya nchi yao.
Utata kuhusu mpaka wetu katika Ziwa Nyasa haujaanza leo. Ulikuwepo tangu wakati nchi zetu mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na kuendelea baada ya Uhuru wa nchi zetu mpaka sasa.
Jambo kubwa lililo tofauti na jipya ni kwamba hivi sasa, nchi zetu mbili zimeamua kukaa mezani na tunalizungumza suala hilo.