23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu afunguka

Jaji Mkuu Othman Chande
Jaji Mkuu Othman Chande

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

SIKU chache baada ya baadhi ya wabunge kuishutumu mahakama kuwa inatumia mamlaka yake vibaya na kuliingilia Bunge, Jaji Mkuu Chande Othman, amesema chombo hicho kisihukumiwe bila kupewa nafasi ya kujibu.

Shutuma za wabunge zilitokana na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kulitaka Bunge kutojadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, jambo ambalo Bunge ililikataa.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kati ya mahakama na vyombo vya habari, Jaji Othman alisema mahakama inatakiwa kupata nafasi ya kujibu pale inapotuhumiwa, na kwamba haitakiwi kuhukumiwa kabla haijapewa nafasi ya kujibu.

“Tunatakiwa kupewa nafasi ya kujibu, mahakama haitakiwi kuhukumiwa kabla haijapewa nafasi ya kujitetea ndiyo maana hata tunaposikiliza kesi lazima pande mbili zisikilizwe ndiyo hukumu itolewe, ikitokea hukumu imetolewa kwa kusikiliza upande mmoja inaweza kufutwa,” alisema.

Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma za majaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusishwa kupata mgawo kutoka katika akaunti ya Escrow, Jaji Othman alisema si wakati wake.

“Mnataka nizungumzia hilo, si wakati wake, leo tuna mjadala mwingine ndugu zangu,” alisema Jaji Othman.

Alisema mkutano wao na wahariri wakuu wa vyombo vya habari umejikita zaidi kuangalia jinsi ambavyo pande hizo mbili zinaweza kufanya kazi kwa pamoja.

Jaji Othman alisema Idara ya Mahakama inataka habari kuhusu mienendo ya kesi na hukumu ziandikwe kwa usahihi, kwani wananchi wanategemea kupata taarifa zilizo sahihi.

Alisema kuna haja ya kupima baina ya uhuru wa mahakama na uhuru wa taarifa kama vile kuruhusu wapigapicha wa televisheni kufanya kazi zao wakati mahakama ikiendelea.

“Kuna vitu vya kuangalia katika kulijadili hilo, kuna haki ya usiri wa haki ya mtu kuficha siri yake, kesi zenye mvuto pekee hasa za madai kupiga picha ili wananchi wajue kinachoendelea inawezekana, lakini kesi za jinai zina matatizo yake.

“Tutajadiliana na kuweka mwongozo na utaratibu utakuwa upi, heshima ya mahakama inatakiwa kulindwa, hapatakiwi kuwapo zogo, tukiruhusu hiyo tunaweza kufika wakati tukajenga katika mahakama zetu mahali pa kukaa waandishi wa habari.

“Tunaamini vyombo vya habari vinaweza kujenga au kubomoa, wananchi wengi wanategemea habari nyingi kutoka kwenu, pamoja na misingi yenu inayotawala utendaji wenu, tunataka kuona Tanzania inakuwa ya amani,” alisema.

Alisema mkutano wake na wahariri, mahakama imepata maslahi makubwa kwa sababu mambo mengi yamejitokeza ambayo kwa namna moja au nyingine yataweza kusaidia kuboresha upatikanaji wa habari kwa wakati.

“Katika mkutano huu mambo muhimu yamejitokeza ambayo mimi na wenzangu tunakwenda kuyafanyia kazi, lengo ni kusaidia waandishi wapate taarifa sahihi, tunalipa kipaumbele. Tumeona kuna ombi la kuanzisha kitengo cha habari, mimi na wenzangu tunakwenda kulifanyia kazi. Na ninawaambia katika mambo haya hakuna jaji anayetaka kupata umaarufu duniani,” alisema Jaji Othmani.

Alisema siku zote majaji huwa hawataki kujulikana. Akitolea mfano alisema nchini Marekani asilimia 59 ya majaji huwa hawatajwi majina yao, licha ya mahakama zake kuwapo karibu miaka 200.

Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama, Ignas Kitusi, alisema mahakama inaangalia utaratibu wa namna ya kumaliza tatizo la watuhumiwa kukaa mahabusu wakati kesi zao zinaendelea na uchunguzi.

“Suala hili ni changamoto kubwa kwetu, kwani jambo hili linahusisha sekta zaidi ya moja. Hakimu au jaji anaweza kusema mtuhumiwa muda aliokaa gerezani unatosha au uchunguzi bado unaendelea.

“Tumeanza kuangalia utaratibu tukabaini tatizo kubwa lipo kwenye mahakama za wilaya ambazo kwa namna moja au nyingine huwa hazina mamlaka ya kusikiliza kesi kama za mauaji,” alisema Kitusi.

Akitoa mfano, Kitusi alisema upande wa Mkurugenzi wa Mashtaka hauruhusu kupeleka mtuhumiwa mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika.

Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema mahakama na habari ni kimbilio la wanyonge na kwamba mahitaji ya wanahabari ni mahakama kuwa wazi kutoa habari kwa ajili ya kuelimisha watu.

“Sisi tutachotafuta ni taarifa tuelimishe watu ili wafahamu kinachoendelea, mahakama nazo zinataka tutoe habari sahihi, kabla ya haya mazungumzo kumekuwa na kutegeana ama kutoaminiana kati ya mahakama na wanahabari.

“Katika mkutano huu tunataka kufunguka kujua kila upande una matatizo gani, suala la kamera kufanya kazi wakati mahakama ikiendelea linajadiliwa, naamini linazungumzika,” alisema Jaji Mihayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles