Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Atuganile Ngwala amesema atashirikiana na serikali kuhakikisha wanaondoa changamoto za kisheria zinazoikabili idara ya mahakama ili wananchi wapate haki zao.
Jaji Ngwala amesema hayo jana baada ya kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa ya Uhakiki wa Mashauri ya Ardhi na Changamoto za Kisheria na Kitaasisi Tanzania Bara iliyotolewa jana na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete wakati wa Mahafali ya 48 ya yaliyofanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema mahakama ni mhimili muhimu katika ustawi wa taifa, kwa sababu wananchi wamekuwa wakiwasilisha malalamiko yao ya kisheria ili waweze kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.
“Mahakama ni mhimili muhimu kwa ajili ya kusikiliza mashauri ya pande zote mbili za walalamikaji na walalamikiwa ili waweze kupata haki zao, hivyo basi, nitashirikiana na majaji wenzangu ili kuhakikisha tunafanya kazi kwa weledi na uadilifu na kutenda haki kwenye mashauri hayo kwa mujibu wa sheria,” amesema Jaji Ngwala.