25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Je tumekuwa Taifa la matukio?

Na SARAH MOSSISAFU hii ni mpya itakuwa inatoka katika gazeti hili kila siku ya Jumatano. “Sauti ya Kisonge” haina unasaba na kundi lolote la siasa ndani na nje ya nchi.

Lengo la safu hii ni kutekeleza majukumu  ya kuhabarisha jamii ya Watanzania popote walipo ndani na nje ya Tanzania.

Mwandishi wa safu hii atatoa nafasi kwa wananchi kushauri na kuelekeza kila jambo litakalogusa jamii yetu ya Watanzania katika nyanja za siasa, uchumi na kadhalika.

Kwa wale ambao watapenda kukosoa kila kitakachoandikwa watakuwa na nafasi kubwa ikiwa lengo ni kujenga zaidi.

Sauti ya Kisonge leo inakuja na tukio ambalo limetikisa nchi baada ya mwanzoni mwa wiki Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais  Dk. John Magufuli kuchukua uamuzi mgumu kwa Serikali kununua korosho yote katika mikoa ya Lindi na Mtwara na kuliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza kazi ya kusomba zao hilo na kupeleka kwenye maghala.

Huu ni uamuzi mgumu ambao haujapata kufanyika tangu Taifa letu lipate Uhuru miaka zaidi ya 55 iliyopita. Uamuzi wa Rais aliutangaza Ikulu juzi katika hafla maalumu ya kuwaapisha mawaziri wapya wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Waziri wa Kilimo

Hatua ya Rais ilitanguliwa na uamuzi mwingine wa kuwaondoa katika nyadhifa zao aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Badala yake Rais akatangaza kumteua Japhet Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo na Joseph Kakunda akamteua kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Uamuzi wa kuwaondoa kwenye nyadhifa zao mawaziri hao ulikwenda sambamba na kuivunja Bodi ya Korosho iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Mama Anna Abdallah.

Safu hii inapenda kuungana na Rais kwa hatua zote alizozichukua, kwani hakuna ubishi kwamba suala la korosho  limeonekana kutaka kuitikisa nchi lakini kwa ushujaa mkubwa hatukufikia huko.

Sekta ya kilimo na viwanda ni muhimu kwa nchi zetu zinazoendelea huku ikiaminika kuwa asilimia 60 ya Watanzania ambao ni wakulima kwa muda mrefu sasa wamekuwa hawafaidiki na kile wanachozalisha kutokana na jasho lao, matokeo wamekuwa ni watumwa au vibarua wa watu wenye fedha.

Hali hii imewafanya hata hao wakulima wa korosho kuwa ni miongoni mwa wakulima wanaofanya kazi isiyo na malipo yanayostahili kutokana na kile wanachozalisha.

Lakini pamoja na uamuzi huu mgumu wa Rais kuitaka JWTZ kuanza kazi ya kusomba na kusambaza korosho na kuipeleka kwenye maghala, wajibu wa Serikali sasa ni kuangalia namna ipi inayofaa kumsaidia mkulima wa korosho ili matatizo kama haya yasiendelee kutokea.

Sifikirii wala sitaki kuamini kwamba uamuzi wa Rais kuitaka JWTZ kusambaza zao la korosho kwenye maghala utakuwa ndiyo mwarobaini wa tatizo lililojitokeza katika msimu huu wa zao hilo, naweza kusema uamuzi huo umefanywa kwa nia njema ya kunusuru na kulinda nguvu za wakulima zisipotee.

Naamini kabisa uamuzi uliofikiwa ni wa muda mfupi, sasa basi naamini Serikali hivi sasa inakuna kichwa kubuni mpango madhubuti na wa muda mrefu wa kuona matatizo yaliyojitokeza katika msimu huu wa mavuno hayajitokezi tena.

Hivi sasa Tanzania tumegeuka kuwa ni  kama vile Taifa la matukio, kila mara yanazuka mambo mapya ambayo huwafanya wananchi kuanza kukaa kwenye vijiwe kupoteza muda na kujadili kwa muda mrefu jambo moja. Hii hali haipendezi na si mustakabali mwema kwa Taifa letu na kwa vizazi vyetu.

Ni lazima viongozi waliopewa nyadhifa mbalimbali wanao wajibu mkubwa kumsaidia Rais kubuni mbinu mbalimbali zitakazoweza kuliondoa Taifa letu kuwa kwenye mrengo wa “Taifa la Matukio” Hii itaondoka ikiwa tu viongozi watakuwa wabunifu kwenye maeneo yao na kusimamia taasisi wanazoziongoza.

Lakini pia wabunge na viongozi walio kwenye nyadhifa na wale wastaafu wenyeji wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, wanapaswa kuisaidia Serikali kutatua kubuni mipango ya muda mrefu ambayo itakuwa ni mwarobaini wa tatizo hili liweze kuwa historia.

Sifikirii wabunge na viongozi hawa watakuwa wao ni chanzo cha tatizo hili kwa maana ya kukaa kimya na kuiacha Serikali ikihangaika. Taifa hili ni letu sote, korosho ni zetu sote na kila kinachopatikana kinatusaidia wote. Hivyo nishauri kwamba huu sio wakati mwafaka wa wao kukaa kimya.

Serikali inasikiliza ushauri wowote wenye lengo la kujenga na sio kubomoa, Huu sio wakati wa kunyoosheana tena vidole. Huu ni wakati wa kutuliza vichwa na kuangalia wapi tunakwenda.

Kwa upande wa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara  hususani kwa wakulima wa korosho nitoe rai kwamba huu ni wakati wenu wa kuonesha uzalendo wa hali ya juu kwa Serikali, kwa kukaa kimya na kusikiliza kauli kutoka kwa Serikali.

Wakati huu ambapo wanajeshi watiifu wakiendelea na kazi waliyotumwa na Taifa ni hekima kwa wananchi kuonesha umoja wao na uzalendo na kuachana kabisa na kauli zitakazoonesha kuwatenganisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,089FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles