25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI LUBUVA ATUNUKIWA NISHANI YA MAPINDUZI

 

NA MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, ametunukiwa Nishani ya Mapinduzi na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Jaji Lubuva ni miongoni mwa watu 74 waliotunukiwa nishani jana, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ambayo yanafikia kilele chake leo visiwani Zanzibar.

Jaji Lubuva alitunukiwa nishani hiyo katika sherehe zilizofanyika Ikulu mjini Unguja.

Katika utumishi wake, Jaji Lubuva aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ kuanzia mwaka 1977 mara baada ya vyama vya ASP na TANU kuungana.

Akiwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Luvuba alishiriki kutengeneza Katiba mwaka 1979 ambayo iliiweka Zanzibar katika mfumo wa kawaida wa kisheria kutoka ule wa awali wa mahakama za wananchi.

Akizungumza na MTANZANIA mara baada ya sherehe hizo, Jaji Lubuva aliishukuru Serikali ya Mapinduzi kwa kutambua mchango wake.

Alisema akiwa visiwani humo, alishiriki kuleta mabadiliko mbalimbali ya kisheria na kueleza kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979 ndiyo iliunda Baraza la Wawakilishi.

“Namshukuru Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Serikali yake kwa kutambua mchango wangu.

“Nimekaa Zanzibar miaka saba, nimeshiriki kuleta mabadiliko mengi ya kisheria wakati ule nikiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi.

“Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979 ndiyo imekuja kutenganisha muhimili wa Mahakama, Serikali na Bunge (Baraza). Wakati ule ulikuwa mfumo wa mahakama za wananchi, vitu vyote vilikua sehemu moja,” alisema.

SMZ imetambua mchango wa kiongozi huyo katika kujenga na kuiendeleza Zanzibar kutoka kipindi hicho hadi Desemba 1983.

Jaji Lubuva ni miongoni mwa kundi la watu 43 waliotunukiwa Nishani ya Mapinduzi, akiwamo Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Agustino Ramadhani, ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles