Narobi, Kenya
Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua (Jaguar) amefikishwa mahakamani leo akituhumiwa kutoa kauli za kichochezi dhidi ya wafanyabiashara Watanzania na raia wa nchi nyingine waishio nchini humo.
Jaguar alifikishwa mahakamani mapema leo Juni 27, hata hivyo amerudishwa rumande hadi kesho mahakama itakapotoa uamuzi iwapo ataachiliwa kwa dhamana.
Hata hivyo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) imeomba Mbunge huyo azuiliwe kwa siku 14 kwa uchochezi na kutoa vitisho dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni.
Mbunge huyo alikamatwa nje ya Ukumbi wa Bunge, kutokana na kauli zake za kibaguzi akiwataka wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda wanaoendesha shughuli zao katika masoko mjini Nairobi na miji mingine kuondoka nchini humo ndani ya saa 24.