20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo: NMB endeleeni na kampeni ya upandaji miti kutunza mazingira

Na Gustafu Haule,Pwani

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Dk. Selemani Jafo amepongeza juhudi zinazofanywa na Benki ya NMB katika uhamasishaji wa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni.

Dk. Jafo amesema hatua hiyo  itasaidia utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamekuwa na athari katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kiafya na kiuchumi.

Jafo amesema hayo Aprili 19, 2023 wakati akizindua kampeni ya Utunzaji wa Mazingira na matumizi ya Nishati mbadala uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu iliyopo katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini chini ya ufadhili wa NMB kwa kushirikiana na Serikali.

Amesema kuwa,Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa minne iliyoathiriwa kimazingira kutokana na ukataji miti hovyo kwa ajili ya kuchomea mkaa lakini kutokana na juhudi zinazofanywa na NMB kwa kushirikiana na Serikali imekuwa ni hatua nzuri ya kupambana na athari hizo.

“Niwapongeze wenzetu wa NMB kwa kazi kubwa wanayofanya hasa ya kujitoa kupanda miti katika maeneo mbalimbali kwakuwa naamini wamekuwa wadau wakubwa wa kupambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira,”amesema Jafo.

Aidha, Jafo amewaomba NMB kuendelea na kampeni hiyo kwakuwa kufanya hivyo ni hatua kubwa ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kaimu Meneja wa benki ya NMB kanda Dar es Salaam Seka Urio amesema kuwa tayari walianzisha kampeni ya kutunza mazingira kwa kupanda miti 1,000 huku wakiwa na kauli mbiu ya “Kuza mti Tukutunze”.

Urio amesema kuwa hadi sasa tayari wameshapanda miti katika mikoa nane ikiwemo Dar es Salam, Mtwara, Mwanza, Tabora na Arusha lakini kampeni hiyo inaendelea katika mikoa mingine nchini.

Aidha, amesema kuwa ili kufikia malengo  Benki ya NMB imeanzisha shindano la kupanda miti kwa shule za Halmashauri zote Tanzania ambapo tayari jumla ya Sh milioni 472 zimetengwa kwa ajili mashindano hayo .

Meneja huyo amefafanua kuwa shule itakayopanda miti 2000 na kufanikiwa kutunza asilimia 80 itakuwa mshindi wa kwanza na itazawadiwa Sh milioni 50, huku mshindi wa pili akimudu kupanda miti 1500 na kutunza asilimia 75 atapatiwa milioni 30 na mshindi wa tatu atakayepanda miti 1,000 na kufanikiwa kuitunza kwa asilimia 70 wanapata milioni 20.

“Benki ya NMB imeanzisha kampeni hii kwa kushirikiana na Serikali kupitia Tamisemi, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mazingira na Muungano hivyo tunaomba Shule na wadau wengine kuchangamkia fursa hiyo,” amesema Urio.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Saimon amesema kutokana na mkoa huo kuwa karibu na Jiji la Dar es Salaam imesababisha kuathiriwa zaidi na uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha mkaa mwingi.

Hatahivyo,Saimoni amesema kuwa tangu ilipoanzishwa kampeni ya kutunza mazingira na matumizi ya nishati mbadala tayari  wamepanda miti milioni 9.7 lakini kutokana na juhudi kubwa za NMB anaamini malengo yao yatatimia

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles