ELIZABETH HOMBO Na WALTER MGULUCHUMA -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleiman Jafo amewaweka pabaya wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Paul Makonda, Kilimanjaro, Anna Ngwira na Arusha, Mrisho Gambo, na wasaidizi wao baada ya maeneo yako kufanya vibaya katika uandikishaji wa wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza jana mbele ya Rais Dk. John Magufuli mkoani Katavi, Jafo alimwomba mkuu huyo wa nchi kuridhia pendekezo atakalompelekea endapo baada ya zoezi hilo kwisha, mikoa hiyo haitofikisha asilimia 50 ya uandikishaji wapiga kura.
Jafo alisema kwa tathimini ya siku mbili Oktoba 8 na 9 mwaka huu, kuna mikoa iliyofanya vizuri na mingine imefanya vibaya.
Akitolea mfano Mkoa wa Iringa alisema umefanikisha kuandikisha asilimia 53, Mbeya 34 na Songwe 33.
Akizungumzia mikoa iliyofanya vibaya, Jafo alisema Dar es Salaam kwa siku mbili hizo iliandikisha wapiga kura kwa asilimia nane, Kilimanjaro 12 na Arusha 13.
“Mheshimiwa Rais wewe unafahamu kwamba ajenda kubwa hivi sasa ni ya uchaguzi, naomba uridhie kwamba endapo siku saba zitakuwa zimekamilika halafu kuna mikoa bado itakuwa haijafika hata asilimia 50, nitaomba nipeleke dokezo maalumu kwako.
“Haiwezakani hata kidogo katika maeneo haya tuna wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, tuna makatibu tawala, wakurugenzi, maofisa tarafa, watendaji wa kata hadi wa vijiji, ajenda ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndio unatoa mchakato wa maendeleo.
“Naomba uridhie iwapo kuna watu walizembea nitaleta mapendekezo maalumu kwako,”alisema Jafo.
Ingawa Rais hakujibu hoja hiyo, wakati Jafo akiitoa alionekana kutikisha kichwa ishara ya kwamba anakubaliana na Jafo.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari kutoa tathimini ya uandikishaji, Jafo alisema anatarajia kumwomba Rais Magufuli, kuwachukulia hatua wakuu wa mikoa na makatibu tawala, endapo mikoa yao itashindwa kufikisha asilimia 50 ya uandikishaji wapiga kura.
Alisema zoezi la uandikishwaji kwa wapiga kura lilianza Oktoba 8, limeonesha kuna baadhi ya mikoa ambayo mpaka sasa imefanya vibaya wakati muda wa kuandikisha unaisha Oktoba 14.
Jafo alisema hadi sasa jumla ya watu milioni 5. 8 wameshajiandikisha ambao ni asilimia 20 huku wanaume wakiwa ni asilimia 51 na wanawake asilimia 49.
Kutokana na hilo, aliwataka wakuu wa mikoa kuwahamasisha watu wajiandikishe na watambue uchaguzi huu wa Serikali za mitaa ni roho ya Serikali.
Kuhusu vifaa, alisema vifaa vyote vimefika kwa wakati kwenye Halmashauri zote tofauti na miaka mingine ufanisi umekuwa ni mkubwa.
Mgao wa umeme ulikuwa dili la watu
Kwa upande wake Rais Magufuli alifichua siri ya kuwepo mgao wa umeme nchini kabla hajaingia madarakani mwaka 2015, akisema ulitokana na baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco ambao walikuwa wakifungulia maji kwenye Bwawa la Mtera ili likauke.
Alisema lengo la wafanyakazi hao ilitokana na kula njama na wafanyabiashara waliokuwa wanauza jenereta ili wawape fedha.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizindua mradi wa umeme wa megawati 132 mkoani Katavi, ambao alieleza kuwa utaokoa zaidi ya Sh bilioni 5.5 zilizokuwa zikitumika kununua mafuta kwa ajili ya majenereta ya kufua umeme.
“Dar es Salaam ilifika kipindi kila mtu ana jenereta yaani Dar nzima ikawa inanuka Petroli na Diseli, kwa sababu umeme ulikuwa wa mgao, sasa tulipoingia madarakani tukasema lazima tuupige marufuku huu mgao kwa njia mbadala na ndio maana tukaongeza production ya umeme.
“Pale kwenye Bwawa la Mtrera mvua zilivyokuwa zikinyesha kuna watu walikuwa wanafungulia maji yatoke na baada ya mwezi mmoja wanakwambia maji yamekauka kumbe walikuwa wanalipwa hela na hawa watu wa majenereta,”alisema Rais Magufuli.
Kutokana na hilo, alisema alimwagiza Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani awatumbue wote na baadaye maji hayajakauka katika bwawa hilo.
Mbali na hilo, pia alisema Serikali ilikuwa ikitoa ruzuku ya Sh bilioni 200 kila mwaka kwa ajili ya Tanesco kujiendesha na bado kukawa na mgao, lakini alipoingia madarakani shirika hilo haijawahi kupewa fedha na mgao umeisha.
“Tanesco, Serikali ilikuwa ikitoa ruzuku ya Sh bilioni 200 kwa mwaka badala ya kuzipeleka kwenye hospitali na huduma zingine lakini zilikuwa zikitolewa Tanesco na bado mgao ulikwepo.
“Tanesco napo kulikuwa na majipu, tukatumbua sasa hatupeleki hata senti tano na umeme unawaka, hakuna mgao tena na katika hilo miradi ya Tanesco sasa imesambaa, wakati tunaingia madarakani vijiji vilivyokuwa vimepelekewa umeme vilikuwa 2000 lakini sasa ni zaidi ya vijiji 8100.
“Ni kweli mkoa mpya wa Katavi umekuwa na tatizo la umeme na kwa dunia ya leo na kwa nchi ninayo plan (ninayopanga) ya viwanda huwezi ukawa na umeme wa jenereta.
“Matumizi ya mafuta kwa ajili ya kuwasha jenereta ili utengeneze umeme yamekuwa makubwa ni Sh bilioni 6.5 kila mwaka inapotea na makusanyo ni Sh bilioni 1.
“Kwa hiyo mnatumia Sh bilioni 5.5 sasa kwa maisha ya leo lazima kila kitu kibadilike,” alisema Rais Magufuli.
Mbali na mradi huo, Rais Magufuli alisema kuna miradi mingine ya umeme ukiwemo wa umeme wa bwawa la Nyerere lililoko katika pori la akiba la Selous mkoani Pwani litakalozalisha megawati 2,115,
Mwingine ni mradi wa gridi ya Taifa utakaounganishwa kutoka Zambia utakaozalisha megawati 400 na kupita Katavi.
Alia na wakimbizi
Katika hatua nyingine aliwataka wakimbizi kutoka Burundi ambao wako katika makambi mkoani humo, kujitathimini kwa sababu wengine wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kihalifu.
“Burundi pameshatulia msidanganywe na watu, wako wanaotaka kuwafanyia ninyi kama biashara, wengine wanawaambia eti ukikimbilia huku utalipwa hela, ni uongo mtupu yaani wewe ukimbie nchi yako halafu ukimbilie nchi nyingine ikupe hela?
“Ni lazima ndugu zangu mnaotoka nchi jirani mkajitathimini, hatuwafukuzi lakini ni lazima tuwaambie ukweli najua ujumbe umefika,”alisema Rais Magufuli.
Ataka Watanzania kuzaa
Pia aliwataka Watanzania kutumia maji katika mojawapo wa mto mkoani Katavi ambao wakinywa maji yake wanazaa mapacha ili Tanzania iwe na watu wengi.
“Ni bahati mbaya tu mke wangu amezeeka na mimi tungeenda kunywa hayo maji, kwa hiyo niwaombe mawaziri na waandishi nendeni mkayachote hayo maji mnywe ili mzae mapacha kwa sababu tutakuwa na watu wengi.
“Na nchi ikiwa na watu wengi ndio maendeleo msidanganyike kuwa nchi ikiwa watu wengi hakuna maendeleo, Nigeria ina watu wengi na ina mtaji mkubwa na hasa ukiwa na watu wanaofanya kazi. Ziko nchi huko wamebaki wazee tu maandiko yote yamesema mkazae kama mchanga.
“Najua Waziri wa Afya hafurahii hili, lakini mimi nataka mzae nikimaliza kipindi changu basi mfunge kuzaa, lakini wakati wangu zaeni kweli kweli, vyakula vipo na elimu ni bure kwanini msizae,”alihoji Rais Magufuli.
Awali, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema mradi huo ulianza Mei mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Mei mwaka 2020.
Aidha alisema mradi huo utagharimu Sh bilioni 137 na ulianza kwa kujenga kituo cha kusambaza umeme kitakachofungwa mashine mbili za megawati 50 kila moja.
“Kazi ya pili ni kujenga njia ya umeme ya Kilovolti 132 kutoka Kiloleni, kupita Inyonga na Ipole mpaka hapa. Mradi huu utajengwa kwa miezi 10.
“Ni matumaini yetu mpaka Mei mwakani utakuwa umekamilika ili wananchi wa Katavi na maeneo yanayozunguka wataanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa na kuacha kutumia mafuta,” alisema Dk. Kalemani.