Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameuagiza uongozi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), kuwasiliana na uongozi wa polisi kuona kama kutakuwa na uwezekano wa kutumika kwa taa za barabarani zilizo kwa mfumo kuongozea magari hayo na si askari kama ilivyo sasa.
Jafo ametoa agizo baada ya kutembelea mfumo wa mabasi ya Dart mbele ya Mtendaji Mkuu wa Dart Mhandisi Ronald Rwakatare, alisema kitendo cha askari trafiki kuongoza magari katika barabara za mfumo huo zinasababisha magari hayo kutofika kituoni kwa wakati.
Alisema malalamiko mengi yanayojitokeza sasa kutoka kwa abiria kuhusu mabasi hayo kutofika vituoni kwa wakati yametokana na mfumo wa magari hayo kuingiliwa na askari wa trafiki wanaoongoza katika taa.
“Unakuta mabasi yanashusha abiria Kivukoni na kuna kundi la abiria wanaohitaji kwenda moja kwa moja Kimara, lakini hayachukui abiria, jambo hili linapaswa kurekebishwa kwani linasababisha kero kwa abiria,” alisema Jafo.
Jafo ambaye alitembelea vituo vya Morocco na Kivukoni, alisisitiza umuhimu wa kutumia taa za kuongozea magari barabarani ili mfumo wa mabasi yaendayo haraka uweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.
Mbali na hilo, Waziri huyo pia aliongelea vitendo vya waendesha bodaboda kukatiza katika barabara za mfumo na kuhatarisha usalama wao na abiria wanaotumia usafiri huo.