28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

ISRAEL YAWASHIKILIA WAPALESTINA 6,500 MAGEREZANI

RAMALLAH, PALESTINA


TAIFA la Palestina jana limeadhimisha Siku ya Wafungwa wa Kipalestina, huku zaidi ya raia wake 6,500 wakishikiliwa katika magereza ya Israel, 350 miongoni mwao wakiwa watoto.

Kwa mujibu wa taasisi ya Kipalestina inayoshughulikia masuala ya wafungwa, vitendo hivyo vimekuwa vikitokea tangu uvamizi wa Israel katika maeneo ya Palestina mwaka 1948.

Imesema ufungaji jela Wapalestina umekuwa sera, njia na chombo cha kuwakandamiza na kuwadhibiti wananchi wa Palestina na kueneza woga na hofu miongoni mwao.

Mbali ya vitendo vya ufungaji jela mara nyingi bila sababu, tangu mwaka 1948, taasisi hiyo imekadiria watu waliowahi kukamatwa na Israel ni zaidi ya milioni moja.

Tayari idadi ya wafungwa katika magereza ya Israel imefikia 6,500, miongoni mwao watoto 350, wanawake 62 na wabunge tisa.

Miongoni mwao 500 walikamatwa na kufungwa bila kushtakiwa, 1,800 ni wagonjwa huku 700 wakihitaji uangalizi wa haraka wa kimatibabu na waandishi wa habari wakiwa 19.

Aidha mateka wengine 48 wako gerezani tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita na wengine 25 tangu robo karne iliyopita na 12 wako jela tangu miaka zaidi ya 30 nyuma.

Wengine 29 ni miongoni mwa mateka wa zamani zaidi waliokamatwa tangu kabla ya Mkataba wa Oslo, ambao walipaswa kuachwa huru katika awamu ya nne Machi 2014.

Lakini utawala wa Israel ulikataa makubaliano hayo na kuwaweka mateka katika magereza yake.

Aidha Wapalestina 214 waliuawa tangu mwaka 1967 ambao 72 miongoni mwao wakati wakiwa mikononi mwa wachunguzi, 60 wamekufa kwa kunyimwa matibabu huku 75 wakiuawa kwa makusudi.

Bunge la Israel, Knesset lilipitisha sheria nyingi za kibaguzi, ikiwamo sheria ya kuwaadhibu mateka wanaogoma kula ya mwaka 2015.

Sheria hiyo inaruhusu kulishwa kwa lazima kwa njia ya sindano, sheria kali ya wanaorusha mawe ambayo inailazimisha mahakama kumhukumu mshtakiwa kwenda jela kati ya miaka miwili hadi minne wakiwamo watoto chini ya miaka 14.

Baraza la Taifa la Palestina mwaka 1974 wakati wa kikao cha kawaida kinachofanyika Aprili 17 ya kila mwaka ilipitisha siku hiyo kuwa ya kitaifa.

Lengo ni kuwaenzi mateka kwa kujitoa kwao mhanga, kuwasaidia na kuunga mkono haki yao ya kuwa huru, pia kusimama karibu nao na wapendwa wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles