TEHRAN, IRAN
RAIS Hassan Rouhani ameituhumu Marekani kupanga njama ya kutumia shinikizo la kiuchumi kuipindua Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika hotuba yake aliyoitoa akiwa kwenye Mkoa wa Kaskazini wa Gilan, Rouhani alisema Iran haiko katika vita ya kiuchumi na kisaikolojia na Marekani na washirika wake.
Mvutano kati ya Iran na Marekani ulianza upya baada ya Rais Donald Trump kuingia madarakani kisha kuiondoa nchi hiyo kutoka katika makubaliano ya mwaka 2015 yaliyofikiwa kati ya mataifa yenye nguvu duniani na Iran.
Makubaliano hayo pamoja na mambo mengine yalidhibiti shughuli za nyuklia za Iran na kuiondolea vikwazo.
Lakini Trump alisema makubaliano hayo yaliyoingiwa wakati wa utawala wa mtangulizi wake, Barack Obama yana upungufu.
Alisema ni kwa sababu hayakudhibiti mpango wa Iran wa makombora ya masafa marefu au msaada inaotoa kwa wanamgambo wenye chembe za kigaidi nchini Syria, Lebanon, Yemen na Irak.
Kwa sababu hiyo, Marekani ilirejesha vikwazo vyake dhidi ya Iran ambavyo vilikuwa vimeondolewa mwaka 2016 kufuatia mkataba huo.