Mkutano wa 140 wa Baraza la Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) umelaani vikali mateso, vitisho na ukiukwaji wa haki za binadamu wa wabunge kote duniani.
Taarifa ya IPU iliyotolewa huko Doha, Qatar, kunakofanyika mkutano huo imesema hayo ikinukuu taarifa ya kamati ya haki za binadamu za wabunge ya IPU ambayo ina haki za kipekee za kusaidia wabunge walio hatarini.
Kauli ya kamati hiyo inafuatia uchunguzi wake wa visa 187 kwenye nchi za Uturuki, Venezuela, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Maldives, Ufilipino, Uganda, Cote d’Ivoire, Indonesia, Niger, Brazil, Ecuador na Mongolia.
Asilimia 84 ya wabunge hao ni kutoka upinzani ilhali asilimia 25 ni wanawake.
Venezuela
Nchini Venezuela, kamati imechunguza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wabunge 64 kutoka upande wa upinzani ambao wamekumbwa na ukamati holela, kuswekwa rumande bila kesi zao kusikilizwa na kuzuia kutekeleza majukumu yao ya kibunge.
Wabunge hao wanapinga serikali ya Rais Nicolas Maduro na licha ya kupata idadi kubwa ya viti bungeni kufuatia uchaguzi wa mwaka 2015, bado hawajapatiwa fedha ili kufanikisha shughuli zao.
Uturuki
Zaidi ya mashtaka 600 ya uhalifu na ugaidi yanakabili wabunge 61 wa chama cha HDP tangu mwezi Disemba mwaka 2015 wakati katiba ilivyofanyiwa marekebisho ili kuondoka kinga dhidi ya wabunge wote.
Wabunge 10 hadi sasa wanashikiliwa korokoroni.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
Angalau huko DRC, kuna nuru kwa kuwa wabunge wawili wa zamani waliokuwa wanashikiliwa kwa muda mrefu wameachiwa huru, kitendo kinachopongezwa na IPU.
Wabunge hao ni Franck Diongo na Eugène Diomi Ndongala ambapo tangu mwaka 2012, kamati ya IPU imekuwa ikisaka kuachiliwa huru kwa Ndongala na mwaka 2016 kwa Diongo.
Ufilipino
Nchini Ufilipino, IPU bado ina wasiwasi mkubwa kwa kuwa miaka miwili tangu kukamatwa, Seneta Leila de Lima bado yuko korokoroni licha ya kutokuwepo kwa ushahidi wowote wa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
IPU inatoa wito kwa mamlaka nchini humo zimwachie huru haraka na mchakato wowote wa kisheria dhidi yake utupiliwe mbali.
Umoja huo wa mabunge duniani unasema kuwa iwapo hilo halitafanyika, utaitisha msimamizi wake wa mashtaka ili aweze kufuatilia uhalili wa mchakato wa kesi inayoendelea.