JAKARTA, INDONESIA
SERIKALI ya Indonesia imeionya Australia kuwa kuuhamisha ubalozi wake nchini Israel kutoka Tel Aviv kwenda Yerusalem kunaweza kuhujumu mchakato wa kutafuta amani kati ya Palestina na Israel.
Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison alisema nchi yake iko wazi kubadilisha msimamo wake kuhusu kuutambua Yerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Lakini amesisitiza bado nchi yake inajizatiti kwa suluhisho la kuwa na mataifa mawili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyadh al Maliki amesema anatumaini Australia itatafakri upya uamuzi wake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Retno Marsudi amesema amewasilisha mtizamo wa nchi yake kwa Australia unaoihimiza pamoja na nchi nyingine kuendelea kuunga mkono mchakato wa amani na kutochukua hatua zozote zitakazouhujumu.
Mabalozi wa nchi 13 za Kiarabu wamekutana na kukubaliana kutuma waraka wa pamoja kwa Australia kuelezea wasiwasi wao kuhusu hatua ya kutaka kuuhamishia ubalozi wake Yerusalem.