27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

INATIA AIBU MISS TANZANIA KUDAI ZAWADI

Na CHRISTOPHER MSEKENA

BAADA ya kutoka kwenye kifungo kilichotokana na kukiuka taratibu za mashindano ya urembo, shindano la Miss Tanzania lilirejea kwa kishindo mwaka jana likiwa limebeba matumaini mapya kwa Watanzania.

Jamii ilichoka kushuhudia vibweka ambavyo vilionekana dhahiri ukiukwaji wa taratibu za mashindano kiasi kwamba Serikali ililiona hilo na kufikia uamuzi wa kulifungia shindano kwa lengo la kurudisha hadhi yake.

Kiu kubwa ya wadau wa tasnia ya urembo ilikuwa ni kuona jukwaa la Miss Tanzania linakuwa daraja la kuzalisha ajira kwa warembo makini wenye haiba kama ya kina malkia wa nguvu, Hoyce Temu.

Warembo kama hao walipatikana kutokana na taratibu za mashindano ya urembo kufuatwa vizuri na kama tunavyojua haki ikitawala basi hakuna jambo linaloharibika.

Sasa shindano lilipofungiwa na baadaye kufunguliwa nilitamani kuona mabadiliko makubwa ndani ya Miss Tanzania hasa katika mambo yaliyolitia doa na kupunguza kasi ya kulifikia taji la urembo wa dunia.

Turudi kwenye hoja yangu, wiki hii mrembo aliyeibuka mshindi wa shindano la Miss Tanzania mwaka jana, Diana Edward, aliweka wazi kutokabidhiwa zawadi zake kama ilivyotakiwa.

Kwanini hakupewa zawadi licha ya jamii kuaminishwa kuwa mshindi wa shindano hilo angepata zawadi ya gari na kiasi flani cha fedha. Leo mrembo wetu anaibuka na kudai hajapata zawadi zake, hii ni aibu.

Ikumbukwe kuwa, Diana ndiye aliyekwenda Marekani kwenye shindano la urembo wa dunia kuiwakilisha Tanzania. Alifanya vizuri kwenye shindano hilo na kama asingefanyiwa hujuma na yule mrembo wa Kenya basi angekuwa kwenye nafasi nzuri.

Mpaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) linaibuka na kuwataka waandaaji wa shindano hilo kumkabidhi mrembo wetu zawadi zake ni jambo la aibu. Tukio hili linaweza kuwa dogo lakini linapunguza heshima ya shindano.

Siyo kila mtu anaweza kuwaelewa waandaaji wa Miss Tanzania, wapo watu watakaosema ubabaishaji umeingia kwenye kamati ya shindano, kitu ambacho hakipendezi na si jambo la afya kwa uhai wa tasnia ya urembo nchini.

Nimalize kwa kusema kuwa shindano kubwa kama Miss Tanzania halipaswi kuchukuliwa poa hasa katika udhamini, ingawa waandaaji wa shindano hawajaweka wazi sababu za kutompa mrembo wetu zawadi zake ila inaonyesha wazi kuna tatizo nyuma ya pazia baina yao na wadhamini. Mpeni Diana zawadi zake tuijenge pamoja tasnia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles