Na ANNA RUHASHA
SHULE ya Msingi Bongonya wilayani Sengerema   inakabiliwa na upungufu wa walimu  baada ya  baadhi yao   kuihama shule   kwa madai ya  kukithiri  ushirikina.
Kwa mujibu wa walimu hao, hali hiyo  imekuwa ikichangia wanafunzi kuanguka ovyo pamoja na kuwapo fisi wengi.
Hayo yalielezwa   wakati wa  ziara ya Mbunge wa   Sengerema, William Ngeleja  kukagua shughuli za maendeleo  akiwa na Kaimu Ofisa Elimu Msingi  wa Wilaya hiyo, Theobadia Katama.
Ilielezwa kuwa   shule hiyo hivi sasa ina   walimu  saba  wakiume  na   upungufu wa walimu 10.
Katama alisema   kilichosababisha  shule hiyo kukosa walimu ni pamoja na waliokuwapo kuomba uhamisho wa lazima kutokana na mazingira   shuleni hapo ya   kuanguka  wanafunzi na kuzingirwa na fisi katika maeneo wanayofanyia kazi.
‘‘Ndugu wananchi  hapa  shuleni tulikuwa na walimu wengi lakini waliomba uhamisho baada kuhofia usalama wa maisha yao.
“Hao walimu walikuwa  wanasema wasipohamishwa  wanaacha kazi… haka  kamchezo kaishe vinginevyo hatutapata walimu wa kutosha hapa, ’’ alisema Katama.
Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Elias George, alisema shule   ina   wanafunzi 800 na     walimu wamekuwa na mzigo mkubwa wa kukabiliana na vipindi.
Alisema  kila mwalimu ana zaidi ya vipindi 30  hivyo akaiomba a serikali kutatua changamoto hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Stansilaus Costantine alisema  matukio ya kuanguka yamekuwa yakiwakuta wanafunzi na siyo walimu.
Alisema  walimu walitumia kigezo hicho labda kwa kuona shule haina miundombinu rafiki kwao.
Mbunge wa   Sengerema,william Ngereja,  akizungumza  na wananchi wa kijiji hicho   alisema tatizo hilo litatatuliwa kwa dua na sala za mashekh na mapadri kukemea mapepo hayo.