CHRISTINA GAULUHANGA Na BOSCO MWINUKA (TURDACO)-DAR ES SALAAM
MANISPAA ya Ilala imetenga Sh milioni 300 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kuweka taa zinazotumia umeme wa jua (sola) ili kuwezesha wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo na baadhi ya mitaa kufanya kazi kwa saa 24.
Ufungaji huo wa sola ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alilolitoa Februari 28, mwaka huu alipokutana na wafanyabiashara wa Kariakoo.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana Dar es Salaam, Ofisa Habari na Elimu kwa Umma wa manispaa hiyo, Tabu Shaibu, alisema kamati maalumu iliyoundwa kwa utekelezaji wa agizo hilo, ilishauri kufunga taa hizo.
Tabu alisema kuwa Serikali imepanga mpango wa kubadilisha utaratibu wa kufanya biashara katika eneo la Kariakoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24 kama yalivyo masoko mengine makubwa duniani.
Alisema baada ya agizo la Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliunda kamati maalumu ambayo nayo iligawa majukumu na baadhi ya mapendekezo ili biashara hiyo iwe endelevu.
“Kamati imegawa majukumu kwa watu mbalimbali, sisi Ilala tumepewa jukumu la kuhakikisha tunawasha taa ambalo tayari tumeanza utekelezaji na tumeliweka kwenye bajeti yetu,” alisema Tabu.
Kaimu Meneja wa Soko la Kariakoo, Donald Sokoni, alisema tayari wamefanya ukarabati wa miundombinu ya vyoo, usafi na wameongeza taa 20 kuzungusha jengo la soko hilo.
“Kwa sasa tumejiandaa vyema kupokea soko la saa 24, kwani tumefanya maboresho pamoja na kuweka mikakati ya ulinzi,” alisema Sokoni.
Alisema hata hivyo wakati wanapokea agizo hilo, wanaanza kuangalia changamoto iliyopo mbele yao ya magari ya mizigo kugongana na wafanyakazi hao baada ya muda kuongezwa.
“Soko letu la shimoni linafanya kazi zaidi ya kupokea mazao kwa saa 24, hivyo tuna wasiwasi wa kuwapo kwa msongamano hasa nyakati za usiku,” alisema Sokoni.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Kaskazini, Kondo Thabith, alisema tayari wamesambaza barua 190 kwa wamiliki wa majengo na kuwapa miezi mitatu ili waweze kutekeleza agizo la upakaji rangi.
Alisema hata hivyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mgongano wa sheria na maagizo, unaosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kutekeleza kwa wakati.
“Wakati agizo linakuja wananchi wapake rangi majengo yao, halmashauri inahitaji hadi uwe na kibali ambacho kinaanzia Sh 100,000 na kuendelea, ambazo wengine wanadai hawana fedha hizo jambo ambalo linaleta changamoto katika utekelezaji,” alisema Thabith.
Alisema changamoto nyingine wanayokumbana nayo mtaa huo ni kuwa na stoo nyingi kuliko maduka, hivyo nyakati za usiku magari huingia kwa wingi kushusha mizigo.
Pia alisema baadhi ya wafanyabiashara hufanya biashara kwa saa 12 na kuondoka, hivyo kitendo cha kuongeza muda kinaweza pia kuleta mgongano kwa sababu ya uhaba wa maeneo baina ya wafanyabiashara hao.