WASHINGTON, MAREKANI
IKULU ya Marekani imerejesha vibali vya mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la CNN, Jim Acosta wiki mbili baada ya kuvifuta kufuatia majibizano baina yake na Rais Donald Trump alipozungumza na waandishi wa habari.
Hiyo pia imekuja siku kadhaa baada ya jaji kuamrisha utawala wa Trump kumrejeshea mwandishi huyo kibali hicho.
Hata hivyo katika kile kinachoonekana kudhibiti waandishi wadadisi kama Acosta, Ikulu ya Marekani ilitangaza sheria mpya, Â ambazo zitaongoza mikutano ya baadaye.
Hiyo ni pamoja na swali moja kwa kila mwandishi wa habari huku maswali mengine zaidi yakiulizwa  kwa ruhusa ya rais au ofisa wa Ikulu, kwa mujibu wa barua iliyotumwa.
Lakini pia barua hiyo   ilionya kuwa hatua zaidi zitachukuliwa dhidi ya Acosta ikiwa hatafuata sheria hizo mpya.
Akizungumzia uamuzi huo wa kurejeshewa vibali vyake, Acosta alisema anataka kurudi kuripoti Ikulu.
Wakati Trump akizungumza na  waandishi wa habari, mfanyakazi wa lkulu alijaribu kuchukua kipaza sauti kutoka kwa Acosta ambaye alikuwa akiendelea kumuuliza maswali  Trump.
Trump alimuita Acosta mtu mbaya na mwandishi huyo akapokonywa kibali cha  kuingia Ikulu siku moja baadaye.
Ikulu pia ilitoa maelezo ikidai Acosta alifutiwa vibali kwa kumwekea mikono yake mwanamke  aliyekuwa akifanya  kazi yake.
CNN ilifungua  kesi mahakamani kutaka vibali vya Acosta virejeshwe,  hatua ambayo iliungwa mkono na vyombo vingine vya habari kikiwamo televisheni ya Fox News, ambayo inafahamika kumuunga mkono Trump.
Jaji alipotia uamuzi wake kuhusu suala hilo la Acosta,  alisema Ikulu  haikuwa na sababu za kutosha za kufuta vibali hivyo.