Manchester, England
KLABU ya Manchester United imemzuia mchezaji wao mpya Odion Ighalo kufanya mazoezi pamoja na wachezaji wenzake kwenye Uwanja wa AON Complex, kutokana na kumuhofia kuwa na virusi vya Corona.
Mchezaji huyo alijiunga na Manchester United wakati wa dirisha dogo la usajili wakati wa Januari mwaka huu akitokea klabu ya Shanghai Shenua ya nchini China kwa mkopo.
Ighalo mwenye umri wa miaka 30, raia wa nchini Nigeria, alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka jana.
Virusi hivyo vya Corona vinapatikana nchini China, hivyo United wanahofia mchezaji huyo kuwa navyo kwa kuwa alikuwa anacheza soka nchini humo na aliondoka wakati tayari vimegundulika.
Hata hivyo, inasemekana kuwa mji wa Shanghai ambao alikuwa mchezaji huyo hadi anaondoka hapakuwa na dalili yoyote ya mtu kupatwa na virusi hivyo, huku ikidaiwa vimeanza kugundulika katika mji wa Wuhan.
Lakini mchezaji huyo anaendelea na mazoezi chini ya kocha Wayne Richardson kwenye Uwanja wa GB Taekwondo Centre na kuna uwezekano kuanzia leo akaungana na wenzake kwa mara ya kwanza.
Inasemekana kuwa zaidi ya watu 1,100 nchini China wamegundulika kuwa na virusi hivyo, hivyo Ighalo hakuweza kujiunga na klabu ya Manchester United wakati wa maandalizi ya Ligi huko nchini Hispania ambapo walikwenda kuweka kambi.
Hali hiyo ya virusi imesababisha watu washindwe kusafiri kutoka China kwenda nchi zingine au kuingia China, lakini kwa upande wa Ighalo anafanyiwa vipimo vya mwisho kwa ajili ya kujiridhisha.
Mchezaji huyo alisajiliwa na Manchester United siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili ambapo hadi sasa ni siku 15 na hajapata nafasi ya kujiunga na timu katika michezo yao. Kocha Ole Gunnar Solskjaer anaamini mchezaji huyo ataungana na timu wiki hii.