DERICK MILTON-SIMIYU
Naibu Waziri wa Fedha Dkt Ashatu Kijaji ameutaka uongozi wa chuo cha usimamizi wa fedha nchini (IFM) kutumia mfumo wa Tehama katika ufundishaji wa wanafunzi wake ili kukabiliana na changamoto ya watumishi inayowakabili.
Mbali na hilo Naibu Waziri huyo amesema kuwa kutumia mfumo huo wa teknologia, chuo hicho kitapunguza gharama za uendeshaji ikiwa kuongeza ufanisi wa masomo yanayotolewa katika matawi yake yote nchini.
Dkt. Kijaji ametoa kauli hiyo leo wakati akikagua ujenzi chuo hicho tawi la Kanda ya ziwa Mashariki kinachojengwa katika kijiji cha Sapiwi Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa ili chuo hicho kiweze kukabiliana na tatizo la upungufu wa watumishi, lazima kijikite kuwafundisha wanafunzi walioko kwenye matawi yake yote nchini kwa njia ya teknologia ya tehama.
Amesema kuwa kwa kutumia njia hiyo, chuo kinaweza kuwa na wafanyakazi wachache hasa wahadhiri lakini kikaweza kuwafikia wanafunzi wake wote tena kwa wakati mmoja.
“ Mnao uwezo wa kuwafundisha wanafunzi wa hapa Simiyu mkiwa Dar es salaam, Mwanza au Dodoma, nchi yetu tayari inao mkongo wa taifa ambao unawawezesha kutekeleza hili, kwa mfumo huu mtaweza kuwafikia wanafunzi wengi zaidi kwa wakati mmoja,” amesema Dkt Kijaji…..
“ Ikiwa mtatumia teknologia hii itawasaidia wahadhiri kutoa somo moja, wakati mmoja kwa mfanano na hakutakuwa na mwanafunzi hata mmoja atakayelalamika kuwa hajafundishwa jambo fulani au mada tofauti na matawi mengine,” ameongeza Dkt Kijaji.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi huo Makamu Mkuu wa chuo Prof. Thadeo Satta amesema kuwa tawi hilo litaanza kupokea wanafunzi ngazi ya cheti mwezi Oktoba, 2020 na wataanza wanafunzi 300.