Yamoussoukro, Ivory Coast
Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo anatarajiwa kurejea nchini humu leo Juni 17, 2021 kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa mwaka 2011 kwa tuhuma za ghasia zilizosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Rais huyo aliyeshikiliwa na mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC).
Mamlaka za Ivory Coast zimeahidi kwamba atapokelewa kwa heshima zote kutokana na hadhi ya ofisi aliyoshikilia nchini.
Kurejea kwa Gbagbo kunatarajiwa kupiga jeki chama chake cha Ivorian Popular Front ambacho kinakabiliwa na mgawanyiko kwa miaka kadhaa sasa.
Waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wameapa kufanya maandamano atakaporejea.
Ijapo kuwa Gbagbo hatimaye aliondolewa mashtaka yote katika kesi dhidi yake ya ICC tarehe 31 mwezi Machi 2021, bado anakabiliwa na mashtaka nchini Ivory Coast kwa kuhusika na wizi katika Benki Kuu ya taifa hilo la Afrika Magharibi tawi la Abidjan (BCEAO).
Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kuhusika na wizi wa BCEAO mnamo Januari 2018.
Rais Ouattara alimsamehe mtuhumiwa mwenzake katika kesi hiyo lakini hakuwajumuisha watu waliofunguliwa mashtaka katika mahakama za kimataifa.