Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Waandishi wa habari wametakiwa kuibua changamoto ambazo haziwadhalilishi watu wenye ulemavu au kuleta picha mbaya kwa serikali.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Internews kuhusu habari za watu wenye ulemavu, Mkurugenzi wa Huduma za Watu wenye ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Jacob Mwinula, amesema wanahitaji masuala ya watu wenye ulemavu yasikike bila kuathiri ustawi na haki zao.
“Tunahitaji masuala ya watu wenye ulemavu yasikike bayana hivyo tusichoke kuibua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu lakini tuzingatie utu, sheria na miongozo iliyopo nchini,” amesema Mwinula.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Josephine Lyengi, amesema wameanza kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uboreshaji wa sera na sheria mbalimbali zinazolinda watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mkurugezi wa Shirika la Vijana Wenye Ulemavu (YoWDO), Genarius Geisha, amewataka waandishi wa habari kuzingatia utu kwanza na inapobidi kutaja aina ya ulemavu wa muhusika wafanye hivyo kwa lengo la kufikisha ujumbe.
“Lugha tutakayotumia itaonyesha jinsi gani tunaheshimu haki za watu wenye ulemavu, kupitia lugha nzuri tunaweza kuondoa unyanyapaa na hivyo kutengeneza furaha kwa watu wenye ulemavu,” amesema Geisha.
Awali Mratibu wa Programu za Internews Tanzania, Shabani Maganga, amesema mradi wa habari za watu wenye ulemavu ulioanza Februari mwaka huu umeleta mabadiliko makubwa katika jamii ambapo zaidi ya habari 221 zimezalishwa mpaka sasa.
“Viongozi wengi wameitikia wito na kuchukua hatua kwa kutoa msaada kuwasaidia watu wenye ulemavu waliokuwa wamefichwa na baadhi ya vyombo vya habari vimenzisha vipindi vya kudumu vya watu wenye ulemavu,” amesema Maganga.
Aidha Internews imetoa ruzuku kwa mashirika 12 ya watu wenye ulemavu na kati ya hayo sita tayari yameshaanza kutekeleza miradi ambayo itafikia tamati Desemba mwaka huu.