24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali ya Mkapa yapandikiza betri kwa wagonjwa nane wa moyo

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

HOSPITALI ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyoko jijini Dodoma imefanikiwa kupandikiza betri kwa wagonjwa nane ambao mapigo yao ya mayo yalikuwa yameshuka.

Hayo yameelezwa Jumatano Oktoba 26,2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Alfonce Chandika wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za hospitali hiyo pamoja na vipaumbele kwa mwaka 2022-2023.

Dk. Chandika amesema kuna wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yalishuka sana, walihudumiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia maabara hiyo wameweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo.

Amesema hospitali imeanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliobainika kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya moyo ambapo tayari watoto 10 wameshahudumiwa.

Amesema hospitali hiyo imefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya moyo ambapo kuna maabara maalum inayotumika katika kutoa matibabu ya moyo pasipo kufungua kifua.

“Hospitali hii ni ya pili hapa nchini kutoa huduma hii. Tangu huduma hii imeanza kutolewa mwaka 2019, jumla ya wananchi 715 wamehudumiwa kwa kuchunguzwa.

“Wagonjwa 39 waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa vipandikizi na kati ya 39, wagonjwa wawili kati yao walihudumiwa kwa dharura ambapo kama ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza maisha,” amesema Dk. Chandika.

Amesema tangu mwaka 2020, Hospitali imefanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi, hadi sasa jumla ya wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama ya Sh milioni 12.

“Gharama za huduma hii nje ya nchi ni takriban milioni 35. Kwa wagonjwa 56 waliohudumiwa , Serikali imeokoa Sh bilioni 1.28 

“Hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia  mgonjwa upasuaji.

“Huduma hii imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Sh milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya Sh milioni 7,” amesema Dk. Chandika.

Amesema kwa wagonjwa 148,  Serikali imeokoa zaidi ya Sh milioni 850. Katika hatua nyingine Dk Chandika amesema wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, hospitali ilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba ‘oxygen’ .

Amesema Serikali iliwapatia Sh bilioni 1.1 na Sh milioni 400 zilitokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kununua na kusimika mtambo wa kuzalishia hewa tiba, kununua mitungi 560 na gari la kusambazia hewa tiba hiyo katika Hospitali mbalimbali, jumla mradi umegharimu Sh bilioni 1.5.

Amesema mtambo huo una uwezo wa kuzalisha mitungi 400 ndani ya masaa 24, tangu mtambo huu uzinduliwe, Julai 1, 2022, jumla ya mitungi 13,467 imeshazalishwa ambapo mitungi 10,962 imetumiwa hospitali  na mitungi 2,505 ilisambazwa kwenye Hospitali zenye mahitaji.

Amesema uzalishaji wa mitungi hiyo  Hospitalini hapo ndani ya kipindi kifupi, umeokoa zaidi ya Sh milioni 500 na imeongeza mapato ya ndani ya hospitali kwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 75 ambazo Hospitali zingine zinachangia kwa kupelekewa huduma hiyo.

Amesema Hospitali ilipata mgao wa fedha za IMF wa jumla ya Sh bilioni 2.6 kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 ambazo zilitumika kuboresha huduma za dharura.

“Tayari tumeboresha kitengo cha huduma hizo ambapo tumeongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda sita hadi 22, tumenunua Digital X-RAY, tunatarajia kupokea gari za kubebea wagonjwa wa dharura mbili,  kufungiwa vifaa vya kutolea huduma za tiba mtandao na vifaa vya maabara,” amesema Dk. Chandika.

Amesema katika kipindi cha Uviko-19, Hospitali hii ilikuwa ikitumia zaidi ya mitungi 200 kwa siku idadi ambayo ilikuwa ikitumika katika hospitali hiyo kwa mwezi mzima kabla ya mlipuko wa ugonjwa huo, hivyo uwekezaji huu ni wa tija sana.

“Tumejipanga kuanzisha huduma mpya ya upandikizaji wa uroto ambapo kwa sasa tunakamilisha maandalizi, kupitia mapato ya ndani,” amesema Dk. Chandika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles