Aziza Masoud, Dar es Salaam
HOSPITALI ya Rufaa ya Amana imekubwa na uhaba wa damu hali inayotishia uhai wa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata na kuthibitishwa na Mganga Mkuu wa hospitali ya Amana Dk.Meshack Shimwela zinaeleza kuwa hali hiyo imejitokeza siku za hivi karibuni.
Wakati taarifa ambazo gazeti hili limezipata zikidai kuwa ukosefu huo umesababishwa na kuharibika kwa mashine ya kutunzia damu, Dk. Shimwela yeye alisema jambo hilo halifahamu isipokuwa anachojua yeye ni kwamba hospitali yake inakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa damu kwa muda wa wiki moja na nusu sasa.
Kabla gazeti hili halijawasiliana na Dk. Shimwela, baadhi ndugu wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo wakihitaji huduma hiyo ya damu walizungumza na chumba cha habari cha gazeti hili walidai kuwa kwa siku kadhaa sasa wagonjwa wao wameshindwa kuongezewa damu katika hospitali hiyo kwa madai kuwa hakuna damu kwa sasa.
“Ndugu zangu wawili wamelazwa hospitali ya Amana na walipaswa kuwekewa damu tangu juzi(Jumanne) lakini tunaambiwa damu hakuna,”alisema.
Alisema hali hiyo imesababisha mmoja kati yao kufariki juzi jioni huku aliyebaki akiwa na hali mbaya jambo ambalo liliwasukuma madaktari wa hospitali hiyo kumuweka damu juzi jioni.
Akizungumzia hali hiyo Dk. Shimwela alisema; “Ni kweli kuna shida ya upatikanaji wa damu ambayo ni salama,damu tulizonazo bado hatujahakiki kwamba ni salama,tunasubiri majibu ya damu salama ili tuweze kuwawekea wagonjwa,”.
Alisema tatizo la upungufu wa damu katika hospitali hiyo lipo karibu wiki moja na nusu sasa .
“Damu zote tunazokusanya huwa tunapeleka Damu Salama kwa ajili ya kuzithibitisha kama zinafaa kwa kumuwekea mtu ukifanya tofauti na hapo unakuwa umekiuka taratibu.
“Mfano unaweza ukamuwekea mtu damu ambayo haijathibitishwa alafu baada ya mwaka mmoja unashangaa anakuja kulalamika aliwekewa damu yenye HIV mnapata kesi na pia unakuwa haujamsaidia, hii hali hata mimi inanitesa lakini sina njia ya kuwasaidia zaidi ya kusubiri damu salama,”alisema Dk.Shimwela.
Alipoulizwa endapo kuna utaratibu wa hospitali kusaidiwa damu na benki ya damu tofauti nje ya ile waliyopeleka Dk. Shimwela alisema utaratibu huo huwa unatumika na mara nyingi huwa zinatumika damu zinazotoka mikoani.
“Utaratibu upo na mara nyingi damu kutoka mikoani huwa tunazitegemea lakini kama zinakuwa hazipo kunakuwa hakuna namna nyingine,”alisema Dk.Shimwela.
Akzungumzia matatizo ya upungufu wa damu alisema mara nyingi huwapata zaidi wajawazito kutokana na kutokuwa makini na mahudhulio ya hospitali mara tu wanapopata ujauzito.
“Wajawazito wengi wanabeba mimba bila kuangalia hali zao za kiafya,unapotaka kubeba mimba ni vizuri ukaenda hospitali kuangalia kama damu yako inatosha kwa sababu mtoto akiingia naye atatumia damu nyingi,wakishakupima wakiona damu yako ni ndogo wanakupa vidonge wakati unasubiri kubeba ujauzito.
“Lakini hata ukibeba mimba unapaswa kuwahi kwenda kliniki kule unapimwa kila kitu hadi damu yako,wakiiona ni ndogo haitoweza kukutosha na mtoto utapewa vidonge vya kuongeza damu pamoja na kushauriwa kula vyakula vya kuongeza damu kwa kipindi chote cha mimba hadi utakapokaa sawa,”alisema Dk.Shimwela.
Naye Meneja Mpango wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dk. Magdalena Limo akizungumzia taratibu za uthibitishaji wa damu hiyo alisema taasisi hiyo huwa inapokea sampuli za damu kutoka katika kanda sita ambazo zinahudumia mikoa yao husika.
Alisema kwa hivyo ofisi za kanda nazo zinapokea kutoka hospitali na kuzipeleka damu salama baadae zikishapimwa wanawarudishia a majibu ili waweze kujua zipi ni si salama na zipi ni salama waweze kutumia.
“Kwa hospitali ya Amana walipewa majibu ya uniti 39 Jumatano na kama kuna kiasi kilichobaki maana yake bado tunaendelea kukifanyia kazi kwa sababu tunahudumia kanda zote kwa wakati mmoja,”alisema Dk.Limo.
Kuhusu kiasi kinachotolewa kutototesheleza katika hospitali husika alisema ofisi hiyo pia huwa ina utaratibu wa kupokea taarifa ambayo inaonyesha hali ya damu katika hiospitali zote kila siku asubuhi lengo ni kutaka kujua maeneo yenye upungufu na uhitaji wa damu kuhakikisha huduma hiyo inakuwa sawa.
Alipoulizwa kama pengine hali hiyo inatokana na kuharibika kwa mashine, Dk Limo alisema si kweli.