24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali ya Amana yakumbwa na uhaba wa damu

Aziza Masoud, Dar es Salaam

HOSPITALI ya Rufaa ya Amana imekubwa na uhaba wa damu hali inayotishia uhai wa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata na kuthibitishwa na Mganga Mkuu wa hospitali ya Amana Dk.Meshack Shimwela  zinaeleza kuwa hali hiyo imejitokeza siku za hivi karibuni.

Wakati taarifa ambazo gazeti hili limezipata zikidai kuwa ukosefu huo umesababishwa na kuharibika kwa mashine ya kutunzia damu, Dk.  Shimwela yeye alisema jambo hilo halifahamu isipokuwa  anachojua yeye ni kwamba hospitali yake inakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa damu kwa muda wa wiki moja na nusu sasa.

Kabla gazeti hili halijawasiliana na Dk. Shimwela, baadhi  ndugu wa wagonjwa  waliolazwa katika hospitali hiyo wakihitaji huduma hiyo ya damu walizungumza na chumba cha habari cha gazeti hili walidai kuwa kwa siku kadhaa sasa wagonjwa wao wameshindwa kuongezewa damu katika hospitali hiyo  kwa madai kuwa hakuna damu kwa sasa.

“Ndugu zangu wawili wamelazwa hospitali ya Amana na walipaswa kuwekewa damu tangu juzi(Jumanne) lakini tunaambiwa damu hakuna,”alisema.

Alisema hali hiyo imesababisha mmoja kati yao  kufariki juzi  jioni   huku aliyebaki akiwa na hali mbaya jambo ambalo liliwasukuma madaktari wa hospitali hiyo kumuweka damu juzi jioni.

Akizungumzia  hali hiyo Dk. Shimwela alisema; “Ni kweli kuna shida ya upatikanaji wa damu ambayo ni salama,damu tulizonazo bado hatujahakiki kwamba ni salama,tunasubiri majibu ya damu salama ili tuweze kuwawekea wagonjwa,”.

Alisema  tatizo la upungufu wa damu katika hospitali hiyo lipo karibu wiki moja na nusu sasa .

“Damu zote tunazokusanya huwa tunapeleka Damu Salama kwa ajili ya kuzithibitisha kama zinafaa kwa kumuwekea mtu  ukifanya tofauti na hapo  unakuwa umekiuka taratibu.

“Mfano unaweza ukamuwekea mtu damu ambayo haijathibitishwa alafu baada ya mwaka mmoja unashangaa anakuja kulalamika aliwekewa damu yenye HIV mnapata kesi na pia unakuwa haujamsaidia, hii hali hata mimi inanitesa lakini sina njia ya kuwasaidia zaidi ya kusubiri damu salama,”alisema Dk.Shimwela.

Alipoulizwa endapo  kuna utaratibu wa hospitali kusaidiwa damu na benki ya damu tofauti nje ya ile waliyopeleka Dk. Shimwela alisema utaratibu huo huwa unatumika  na mara nyingi huwa zinatumika damu zinazotoka mikoani.

“Utaratibu upo na mara nyingi damu kutoka  mikoani huwa tunazitegemea lakini kama zinakuwa hazipo kunakuwa hakuna namna nyingine,”alisema Dk.Shimwela.

Akzungumzia matatizo ya upungufu wa damu alisema mara nyingi huwapata zaidi wajawazito kutokana na kutokuwa makini  na mahudhulio ya hospitali mara  tu wanapopata ujauzito.

“Wajawazito wengi wanabeba mimba bila  kuangalia hali zao za kiafya,unapotaka kubeba mimba ni vizuri ukaenda hospitali kuangalia kama damu yako inatosha kwa sababu mtoto akiingia naye atatumia damu nyingi,wakishakupima wakiona damu yako ni ndogo wanakupa vidonge wakati unasubiri kubeba ujauzito.

“Lakini  hata ukibeba mimba unapaswa kuwahi kwenda kliniki  kule unapimwa kila kitu hadi damu yako,wakiiona ni ndogo haitoweza kukutosha na mtoto utapewa vidonge vya kuongeza damu pamoja na kushauriwa  kula vyakula vya kuongeza damu kwa kipindi chote cha mimba  hadi utakapokaa sawa,”alisema Dk.Shimwela.

Naye Meneja Mpango wa Mpango wa  Taifa wa Damu Salama   Dk. Magdalena Limo akizungumzia taratibu za uthibitishaji wa damu hiyo alisema  taasisi hiyo  huwa inapokea sampuli za damu kutoka katika kanda sita ambazo zinahudumia mikoa yao  husika.

Alisema kwa hivyo ofisi  za kanda nazo zinapokea kutoka hospitali na  kuzipeleka damu salama baadae zikishapimwa wanawarudishia a majibu ili waweze kujua zipi ni si salama   na zipi ni salama waweze kutumia.

“Kwa hospitali ya Amana walipewa  majibu ya uniti 39 Jumatano na kama kuna kiasi kilichobaki maana yake bado tunaendelea kukifanyia kazi kwa sababu tunahudumia kanda zote kwa wakati mmoja,”alisema Dk.Limo.

Kuhusu kiasi kinachotolewa kutototesheleza katika hospitali husika alisema  ofisi hiyo  pia huwa ina utaratibu wa kupokea taarifa ambayo inaonyesha hali ya damu katika hiospitali zote kila siku asubuhi lengo ni kutaka kujua maeneo yenye upungufu na uhitaji wa damu  kuhakikisha huduma hiyo inakuwa  sawa.

 Alipoulizwa kama pengine hali hiyo inatokana na kuharibika kwa mashine, Dk Limo alisema si kweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles