29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali binafsi kupangiwa bei elekezi

NA VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM



SERIKALI inafanya mapitio ya mwongozo maalum wa bei elekezi kwa gharama za matibabu katika hospitali na vituo vyote vya tiba vinavyomililikiwa na sekta binafsi.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwezesha   watu wa kipato cha chini kupata huduma za matibabu kokote walipo nchini bila  kikwazo cha aina yoyote.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na  Mkurugenzi wa Tiba   Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.

Alikuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Tiba na Uchunguzi wa Maabara Tanzania  (APHFTA).

“Tanzania ni yetu sote, inakua kwa kasi, bila sekta binafsi peke yetu hatuwezi hasa ikizingatiwa kwamba Watanzania wana uhuru wa kuchagua kutibiwa popote pale.

“Tunahitaji kuweka mazingira mazuri katika vituo vyote vya serikali na vya umma.

“Baadhi ya vituo binafsi, gharama zake zipo juu, hilo wizara imeliona na hivi sasa kuna timu inayofanya kazi ya mapitio kuangalia kituo husika maendeleo yake yamefikia wapi.

“Kama kilipewa ‘status’ kwamba kiwe hospitali ya mkoa lakini hawajaweza kutumikia  vema ‘status’ hiyo, hospitali husika itashushwa ngazi kulingana na viwango vilivyowekwa,” alisema Dk. Dorothy.

Alisema hospitali na vituo vya afya binafsi vinachukua asimilia 40 ya vituo vyote nchini hivi sasa.

“Hivyo tunafanya mapitio na bei zao tunatarajia zitakuwa katika ‘range’ (mfumo) ya kawaida, tuna changamoto pale Wizarani, kuna wengine wanapanda ndege kwenda kutibiwa Nairobi.

“Mtu anataka anapotibiwa pawe na sweeming pool, atibiwe, aogelee na aangalie televisheni, apate chai ya maziwa, imekuwa kama hoteli fulani.

“Nasi tunahitaji kuweka mazingira mazuri katika vituo vyote vya umma na binafsi, lakini hiyo haizuii kwamba tusitoe bei elekezi, kila Mtanzania apate huduma.

“Usije ukaniambia kwamba hospitali yako ni ya hadhi ya nyota tano  na kuna mgonjwa anahitaji huduma ya dharura, homa ipo juu ana degedege, humtibu… kwamba unahitaji milioni kadhaa, hapo utakuwa umetengeneza kesi, tutakushughulikia,” alisema Dk. Dorothy.

Alisema pamoja na hayo kila Mtanzania anapaswa kukata bima ya afya kwa sababu  ndiyo mkombozi pekee katika kupata huduma bora za matibabu.

“Hili Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, analipigia ‘kelele’ kila siku.

“Sasa tupo katika ulimwengu wa bima, huwezi kujua utaugua ukiwa wapi,” alisema.

Awali, Dk. Dorothy alisema wizara imekusudia pia kuzikusanya bodi zote za usajili wa hospitali na vituo hivyo vya afya kuwa katika mwamvuli mmoja.

“Wamenieleza kwamba pamoja na mafanikio yote haya, wana changamoto zinawakabili ambazo sisi kama watunga sera serikalini lazima tuyatambue, ikiwamo mazingira ya usajili.

“Tuna bodi na mabaraza mengi ambayo yapo kisheria, lakini yalifaa kwa sheria hizo kwa wakati ule, sasa mambo yamebadilika na yanakwenda kwa kasi, hivyo tayari Waziri Ummy ametoa maelekezo.

“Bodi hizi zinafanya kuwa kitu kimoja, kuanzia sasa tutakuwa na bodi moja, ndani yake kutakuwa na wataalamu mbalimbali itawarahisishia kuboresha huduma zao,” alisema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa APHFTA, Dk. Samwel Ogillo, alisema usajili wa vituo vya afya, maabara na uboreshaji wa vituo vya afya, ilikuwa ni changamoto kubwa kwao.

“Leo (jana) unafungua kituo cha afya unakuta tozo mbalimbali kati ya sita hadi 10 kulingana na huduma mbalimbali ambazo kituo au hospitali inatoa, mazingira haya yanafanya mzigo mkubwa katika kuendesha biashara.

“Hizi kodi ndizo zinafanya hata gharama za matibabu zinakuwa kubwa.

“Kifaa kile kile kinaagizwa nje kwa gharama mara mbili wakati nje ni nafuu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles