24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja ya fedha yaivuruga CCM

Pic-4-1MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema suala la matumizi ya fedha kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa lilikuwapo katika karne nyingi zilizopita.
Kutokana na hali hiyo, amesema anashangazwa na baadhi ya viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulishupalia suala hilo na hata kuwanyooshea vidole wanachama wengine wanaoliona kama geni.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Kingunge alisema ni wazi pamoja na kuwapo kwa suala hilo, lakini halipaswi kuwa ajenda kwa sasa ila kinachotakiwa ni kuangalia namna gani ya kushughulika nalo bila kuwapo mapambano dhidi ya watu wengine.
“Suala la matumizi ya fedha limekuwapo katika historia yetu kama Watanzania na duniani kote, kumekuwa na vitendo vya watu kutumia fedha kwa madhumuni mbalimbali, ikiwamo kupendwa, kukubalika katika jamii.
“Hata kwetu fedha zimekuwa zikitumika kwa malengo ya kuuza haki, wengine wakitaka kupata upendeleo na suala hilo halikufanyika katika uongozi wa awamu ya kwanza pekee bali kuanzia wakati wa utawala wa ukoloni.
“Hivyo ninashangaa kuona hivi sasa ndipo kunaibuka na maneno kama rushwa, mlungula, hongo huku tukilazimisha kuliondoa katika jamii kwa namna ambayo haikutumika kwa wakati ule ambapo tulikuwa wakali na wachungu.
“Suala hili tulikuwa tukilipiga vita mwanzoni kwa uhuru tukiwaeleza wanachama kwamba matukio haya hayakuwa ya kawaida katika vyama vya TANU, ASP na baadaye CCM,” alisema Kingunge.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, alisema suala la rushwa na hongo limekuwapo tangu awamu ya kwanza na hata kabla ya wakati huo, hivyo kwa sasa si rahisi kulizuia kwa maneno.
Kabla ya kuzungumza na MTANZANIA, Kingunge alianza kwa kuzungumzia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha ‘Kumepazuka’ kinachorushwa na Radio One, ambapo aliwataka viongozi kuyaenzi mapinduzi kwa vitendo kwa sababu ndiyo malengo yake.
“Mapinduzi ya Zanzibar katika bara la Afrika ni tukio kubwa mno kwa sababu waliweza kuwaonesha wakoloni kuwa hawataki kudharauliwa wala kunyanyaswa.
“Kutokana na hali hiyo, waliweza kutetea haki yao na kuonesha kuwa sisi wanyonge wa Afrika kuendelea kunyanyaswa na kudharauliwa ni makosa, hivyo basi tuna kila haja ya kuhakikisha kuwa wakoloni wanaondoka kwenye ardhi yetu,” alisema Kingunge.
Alisema kila mwaka Wazanzibari wamekuwa na utaratibu wao wa kuyaenzi mapinduzi hayo kwa vitendo, ndiyo maana wahanga wa mapinduzi haya waliweza kujitolea kwa nguvu zao kuhakikisha kuwa wanapigania haki yao.
Kingunge alisema kipindi kile kamati ya watu 14 iliyokuwa chini ya Seif Bakari iliweza kufanya mambo yote kuhakikisha kuwa mapinduzi yanapatikana.
Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa wanapigania na kurejesha utu wao na ndiyo maana wakadai nchi yao ili waweze kupata madaraka ya kisiasa ambayo yaliweza kukomesha unyonge wa kunyanyaswa Mwafrika.
“Kuwaenzi waasisi wa mapinduzi kwa kufanya kumbukumbu ya mara moja kwa mwaka haitoshi, bali tunapaswa kuendeleza zaidi ili kuonesha kuwa siku hiyo ni muhimu,” alisema.
Akitolea mfano wa Sikukuu ya Desemba 9 ambayo Tanzania Bara ilipata uhuru wake, Kingunge alisema siku hiyo ni muhimu na kwamba inapaswa kuendelezwa kwa vitendo.
Alisema harakati za mapambano ya kupigania uhuru katika baadhi ya nchi kama vile Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda na Congo na nyingine barani Afrika, zote zilikuwa na malengo ya aina moja ambayo ni kukomesha kunyanyaswa kwa Mwafrika, umasikini na maradhi.
“Tunapaswa kujiuliza kuwa harakati za waasisi wetu ambao walikuwa wanapigania uhuru wa Waafrika, je tumezisahau? Waasisi wetu walikuwa wanapigania nini? Ni lazima tukumbuke walipigania nini,” alisema.
Mkongwe huyo, alisema lakini hilo la kujenga mazingira ya kumkomboa Mwafrika linasuasua, vipaumbele vya nchi haviendani na malengo ya kumjengea utu wake Mwafrika na heshima yake duniani.
Januari 3, mwaka huu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba katika sherehe za Maulidi ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga, aliwataka Watanzania kuwaepuka viongozi wanaotafuta uongozi kwa fedha nyingi, kwani wakifanikiwa kuingia madarakani hawataweza kutawala kwa haki.
Mbali na Makamba, pia makada kadhaa wa CCM akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, David Cleopa Msuya, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kwa nyakati tofauri wamekuwa wakilia na rushwa bila kutaja jina la nani anayehusika na vitendo hivyo.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika kile kinachoonekana kutafuta huruma, alilalamikia vitendo vya rushwa na kudai kundi la mafisadi wamekuwa wakimchukia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles