25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hofu yaibuka Marekani kutuma mtambo wa kuzuia makombora

WASHINGTON, MAREKANI

WASIWASI umeibuka barani Asia na kwingineko kutokana na uamuzi wa Serikali ya Marekani kutuma majeshi na mtambo wa kujilinda dhidi ya makombora na meli ya kivita katika eneo la Mashariki, huku uhusiano wake na taifa la Iran, ukiwa kwenye msuguano mkali.

Kwa mujibu wa maofisa wa jeshi la nchi hiyo na kukaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC wanasema meli hiyo ya kivita iitwayo USS Arlington, inayosafirisha magari na ndege, inatarajiwa kujiunga na kundi la kijeshi la USS Abraham Lincoln katika ghuba.

Aidha, wamesema makombora ya US B-52 Bombers pia yamewasili katika kambi moja nchini Qatar, huku Serikali ya Iran ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni kitisho kufuatia operesheni za vikosi vya kijeshi vya Marekani katika eneo hilo.

Marekani imetoa habari chache kuhusu uwezo wa tishio hilo, ambao utawala wa Iran umepinga na kuita ni kama ujinga, ikitaja hatua hiyo ya Marekani kama vita ya kiakili yenye lengo la kuitishia nchi hiyo.

Wakati huo chombo cha habari cha Isna News Agency, kilimnukuu kiongozi mmoja mkuu wa dini, Yousef Tabatabai-Nejad, akisema kuwa ”msafara huo wa Marekani unaweza kuharibiwa na kombora moja pekee.”

Idara ya Pentagon ya Marekani juzi ilisema kuwa haitaki vita na Iran lakini wapo tayari kulinda vikosi vya Marekani na mali yake katika eneo hilo.

“Idara ya ulinzi inaendelea kufuatilia kwa karibu vitendo vya utawala wa Iran,” ilisema katika taarifa.

Iliongezea kuwa mfumo huo wa makombora ambao unaweza kutungua makombora ya masafa marefu na yale ya chini na ndege za kijeshi pia utapelekwa katika eneo hilo iwapo kuna uwezekano wa shambulio lolote.

Maofisa wameambia vyombo vya habari vya nchini Marekani kwamba meli hiyo ya USS Arlington ilitarajiwa kuwasili katika eneo hilo lakini imepelekwa katika eneo hilo mapema ili kutoa uwezo wa amri zitakazotolewa na udhibiti.

Mshauri wa masuala ya usalama nchini Marekani, John Bolton, alisema kupelekwa kwa vifaa hivyo vya kijeshi kutatoa ujumbe wa wazi kwa utawala wa Iran kwamba shambulio lolote dhidi ya mali ya Marekani katika eneo hilo litajibiwa na uwezo mkubwa wa kijeshi.

Idara ya Ulinzi nchini Marekani imesema kuwa meli hiyo ya USS Abraham Lincoln, ilipita kupitia rasi ya Suez siku ya katikati ya wiki hii.

Mwandishi wa BBC anayeshughulikia masuala ya ulinzi na diplomasia, Jonathan Marcus, anasema hilo si jambo la kawaida kwa meli ya kubeba ndege kutumwa katika Ghuba, hatua hiyo itasababisha hofu ya uwezekano wa vita kuepuka kwa ajali ama mipango.

Mwaka jana Rais wa Marekani, Donald Trump, alijiondoa katika mkataba wa nyuklia wa Iran ambao Marekani na mataifa mengine yalikuwa yameingia makubaliano na Iran 2015.

Katika makubaliano hayo, Iran ilikuwa imekubali kupunguza vitendo vyake vya utumizi wa nyuklia na badala yake kuruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia nchini humo kukagua ili waondolewe vikwazo.

Ikulu ya Whitehouse mwezi uliopita ilisema kuwa ingeyaondolea msamaha mataifa matano ikiwemo China, India, Japan, Korea Kusini na Uturuki ambayo yalikuwa yakiendelea kununua mafuta ya Iran.

Wakati huo huo Marekani pia imeliorodhesha jeshi la Iran kuwa kundi la kigaidi. Utawala wa Rais Trump unatumia kuishinikiza Iran kuanzisha mazungumzo ya makubaliano mapya ambayo yatasimamia si tu vitendo vyao vya kinyuklia bali pia mipango yake ya uundaji wa makombora ya masafa marefu mbali na kile maofisa wanasema ni tabia yake ya ukandamizaji katika eneo lote la Mashariki ya Kati.

Vikwazo hivyo vimesababisha kushuka kwa uchumi wa Iran, vikisukuma thamani ya sarafu yake chini mbali na kuwafukuza wawekezaji wa kigeni na kusababisha maandamano.

Iran imetishia kulipiza kisasi kwa kufunga mlango wa Hormuz ambapo mafuta mengi yanayotumika duniani hupitia. Awali Iran wiki hii ilitangaza kwamba imesitisha utekelezwaji wa sheria 2 za makubaliano ya 2015 kutokana na vikwazo ambavyo vimewekwa na Marekani.

Pia ilitishia kuanzisha upya mpango wa kutengeneza madini ya Uranium iwapo vikwazo hivyo vitaendelea katika siku 60 zijazo.

Mataifa yenye uwezo mkubwa barani Ulaya yamesema kuwa yataendelea kuheshimu makubaliano hayo ya Iran lakini yatakataa masharti yoyote ya utawala huo wa Tehran ili kuyalinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles