KLABU ya Yanga jana, ilihitimisha tamasha lake la Wiki ya Mwananchi, kwa kikosi cha timu hiyo kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Kariobangi Sharks ya Ligi Kuu Kenya, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo zilikamilisha dakika 45 za kwanza zikiwa nguvu sawa.
Kwa ujumla, kipindi cha kwanza, timu hizo zilifanya mashambulizi ya kupokezana.
Yanga ilionekana vizuri katika umiliki wa mpira, lakini udhaifu ulikuwa katika kutengeneza nafasi za mwisho ambazo zimeweka kuwapa mabao.
Hali hiyo inaweza kuwa, ilichangiwa na ugeni wa wachezaji wachezaji wake wengi katika kikosi cha timu hiyo.
Kwa nyakati tofauti, wachezaji Sadney Urikhob, Juma Balinya, Papy Tshishimbi na Patrick Sibomana walipoteza nafasi nzuri za kuipa uongozi Yanga kipindi cha kwanza.
Kwa upande
wa Kariobangi, Patrick Ngunyi alishindwa
kutumia nafasi kuifungia bao.
Kipindi cha pili, kilipoanza Kariobangi iliingia na mkakati mpya na kufanikiwa
kuandika bao la kuongoza dakika ya 48 kupitia kwa Patrick Otieno kwa mkwaju
mkali, baada ya mabeki wa Yanga kuchelewa kumdhibiti akiwa ndani ya eneo la
hatari.
Bao hilo, halikuipunguza nguvu Yanga, badala yake ilizidisha mashambulizi kwa lengo la kugomboa.
Dakika ya 56, mwamuzi wa mchezo huo Elly Sasii aliizawadia penalti Yanga, baada ya mchezaji wa Kariobang, Shefan Oyug, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Penalti hiyo ilipigwa na Sibomana dakika ya 57 na kufungia Yanga bao la kusawazish.
Bao hilo ni kama liliiongezea Yanga ari ya kupambana kwani ilizidisha kasi ya kulisakama lango la Kariobangi.
Dakika ya 65, Yanga ilifanya mabadiliko alitoka Mohamed Issa na kuingia Mrisho Ngassa.
Pia ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 83, ambapo alitoka Balinya na kuingia Maybin Kalengo, huku Kariobangi ikimbadilisha Erick Kapaito na kuingia David Simiyu.
Ili kuwapima zaidi wachezaji wake, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alifanya mabadiliko dakika ya 87, alitoka Urikhob na kuingia David Molinga.
Pamoja na mabadiliko hayo yaliyofanywa na kila upande, dakika 90 zilikamilika kwa timu hizo kufungana bao 1-1.
Kabla ya mchezo huo, yalitanguliwa na matukio mengine likiwemo la utambulisho wa wachezaji watakaoitumikia Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano mengine ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wampa jezi Rais Magufuli
Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla pia alikabidhi zawadi ya jezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
Jezi hiyo ilipokelewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Mwisho wa machungu
Dk Msolla alisema kutokana na mikakati ambayo wameifanya ndani ya Klabu ya Yanga, wanachama hawatajutia tena kama msimu uliyopita.
Alisema, mipango yao ni mikubwa na mpaka sasa wamekamilisha asilimia 80 ikiwemo pamoja na usajili kabambe ambao wameufanya.
“Yanga hii mpya sio ya kubahatisha bali mambo mengi yanafanyika kisomi,”alisema Dk Msola.
Alisema ili kuhakikisha kila jambo linakwenda sawa, atahakikisha mipango inakuwa kwenye mfumo na hakuna mali yoyote ya klabu itakayotumika bila kutambulika.
Makambo kusahaulika
Naye Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema kwa namna ambavyo amefuatilia video za nyota wao mpya, raia wa DRC, David Molinga, mashabiki wa klabu hiyo watamsahau aliyekua straika wao , Eritier Makambo.
Alisema, awali walitegemea nafasi hiyo ingezibwa na Mganda Juma Balinya, lakini Molinga mbadala sahihi zaidi wa Makambo.
“Siwezi kumsemea sana kwa vile wananchi hawajamuona lakini hiki ni kisu hatari, kitafunga mabao mengi sana, chamsingi tusubiri tuone kazi yake,” alisema Mwakalebela.