WENGI kati ya wasichana walio katika ndoa ama mahusiano ya muda mrefu ni wepesi sana kujihusisha na vitendo vya usaliti. Hii ni tafiti rasmi. Ni tafiti inayokera na kuumiza ila huo ndiyo ukweli.
Siku kadhaa nyuma niliwahi kulijadili hili suala katika namna ya kuwaasa wanaume kuwa makini na kuacha kuishi kimazoea na wake zao ili kupambana na changamoto hii. Leo nataka tujadili hili suala katika mtindo tofauti kidogo. Leo nataka kuongea zaidi na wanawake.
Japo mwanamke na mwanaume ni binadamu ambao wote hukumbwa na tamaa za kimwili na kuwa na hisia za upendo ila ukweli ulio dhahiri ni kwamba, tamaduni na mazingira ya kidunia yamewapa zaidi mamlaka wanaume kuwaeleza wanawake namna wanavyojisikia juu yao na wanawake wao kubaki na jukumu ama la kukubali ama kukataa matakwa ya wanaume husika.
Kitu hiki kinaweza kutafsiriwa kuwa kimemuweka mwanamke katika kundi la muwindwa huku mwanaume akijiweka katika kundi la muwindaji. Hali hii ndiyo imesababisha wanawake wakumbwe na changamoto zaidi ya kutongozwa (kuhitajiwa na wanaume kwa ajili ya mapenzi) kuliko wanaume.
Kutokana na mwanamke kuwa katika kundi la muwindwa, mara nyingi hujikuta akikutana na wawindaji (wanaume) wakiwa na mbinu na mikakati mbali mbali kwa ajili ya kuwa naye.
Kwa baadhi ya wanawake hali hii huitafsiri kuwa ni kutokana na uzuri wao ama wana bahati sana katika maisha. Kitu ambacho wengi wanashindwa kutambua ni kwamba wakati mwingine wanaume hutongoza hata bila sababu ila hujikuta tu wakitongoza wanawake kwa sababu anaona akiacha kutongoza uanaume wake utashindwa kutafsirika vema.
Wanawake wengi walio katika mahusiano kwa muda mrefu wamejikuta ni watu rahisi sana kuingia katika mitego ya wanaume wanaowatongoza kwa sababu ya kudhani huko nje kuna mambo mengi mazuri, ya kuleta furaha na amani kuliko ndani ya mahusiano yao.
Hii inatokana na ukweli kwamba, wawindaji hao (wanaume) huja na maneno mazuri na ahadi kemkem zinazopunguza ufahamu wa wanawake husika na kuwaona wawindaji hao ndio hasa watu walio wahitaji katika maisha yao.
Wakati wakiwaza haya, wanawake hawa huwa wanasahau kuwa, upya wao kwa wanaume husika pamoja na wao kuwa katika ndoa ama mahusiano na wanaume wengine ndiyo hasa huwa chanzo cha wao kubabaikiwa.
Hii inatokana na ukweli kwamba, wanawake walio katika ndoa huwa siyo wasumbufu sana kama wanawake wengine wasio katika ndoa.
Tafiti zinajuza, kwa sababu nia ya wanaume wengi wenye kuwatongoza wau walio katika mahusiano huwa ni tamaa za mwili za muda mfupi, hufurahia maisha na wanawake hawa kwa sababu huwa hawaulizii ulizii sana suala la kutaka kuolewa.
Pia uzuri wa wanawake hawa walio katika ndoa ama mahusiano ya muda mrefu huwa na shida na vitu vidogo vidogo tu kwa sababu majukumu yote ya msingi huwa yanamalizwa na waume zao.
Wakati fikra za wanaume hawa wanaotoka na wanawake walio katika ndoa huwa ni mahusiano ya muda mfupi ila ukweli ni kwamba wanawake wenyewe huwa wanajikuta wakitopea sana kwa hawa wanaume na kujikuta wakianza visa na dharau kwa wanaume zao kwa kuona kama wameishiwa ama watu wasio wa kisasa sana.
Matokeo yake hujikuta wakisababisha migogoro mikubwa katika ndoa zao ambayo ama italegeza thamani na hadhi ya mahusiano yao au kuvunja kabisa ndoa zao kitu kinachowapelekea baadaye kujikuta katika majuto makuu.
Ni vema wanawake wakatambua ni rahisi sana kwa aliye ndani ya nyumba kutamani kutoka nje ila jua thamani na hdhi ya binadamu hupatikana akiwa anaishi ndani na siyo nje kama miti ama matunda.