25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

HII YA KENYA BALAA

NAIROBI, KENYA

UAMUZI wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, kuufuta uchaguzi uliompa ushindi Rais aliye madarakani aliyekuwa akiwania kipindi cha pili, Uhuru Kenyatta, kunaifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza barani Afrika kwa matokeo ya urais kufutwa na mhimili huo.

Kwa sababu hiyo uamuzi huo wa Mahakama unavunja maandalizi ya Kenyatta kuapishwa Septemba 12 mwaka huu, kwani kwa sasa atalazimika kuingia kwenye maandalizi ya uchaguzi wa marudio kwa ajili ya kukabiliana na mpinzani wake wa karibu ambaye pia ni kiongozi wa Muungano wa upinzani, Nasa, Raila Odinga ambapo Mahakama imeamuru ufanyike ndani ya siku 60.

Katika uchaguzi ambao Mahakama imeufuta ambao ulifanyika Agosti 8 mwaka huu, Kenyatta alipata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga wa muungano wa Nasa aliyepata kura 6,762,224 sawa na 44.74%.

Licha ya jana kuwa ni sikukuu ya Eid El Haji, lakini Mahakama bado ililazimika kuingia kazini kuhakikisha kesi hiyo iliyofunguliwa na Raila inamalizika ndani ya muda wa kikatiba uliopangwa.

Uamuzi wa Mahakama ulisomwa jana na majaji sita, ambapo wanne walikubaliana  na hoja zilizowasilishwa na Nasa wakati majaji wawili walikubali hoja za Tume ya Uchaguzi, Chama cha Jubilee na wanasheria wa Uhuru Kenyatta.

Mahakama hiyo imesema kwamba, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), iliendesha uchaguzi usiokuwa wa haki na zoezi la kukusanya matokeo halikufanywa kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Jaji Mkuu David Maraga, Makamu wake, Philomena Mwilu, Jaji Smokin Wanjala, Isaac Lenaola, waliafiki pingamizi lililowasilishwa na muungano wa upinzani wa Nasa kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na haki kwa mujibu wa Katiba.

Hata hivyo, Jaji Njoki Ndung’u na Jackton Ojwang’, walipiga kura ya hapana dhidi ya pingamizi la Nasa.

Pamoja na hilo, katika kesi hiyo alikosekana Jaji Mohammed Ibrahim, ambaye anaugua hivyo kushindwa kushiriki na kuwa sehemu ya hukumu ya kesi hiyo.

Majaji wote wanne wamesema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imeshindwa kuthibitisha matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Akizungumza mahakamani hapo, Jaji Mkuu, David Maraga, alisema IEBC iliendesha uchaguzi kinyume cha Katiba kiasi cha kuathiri matokeo ya uchaguzi.

Uamuzi huo wa Mahakama ambao umetajwa kama ni uamuzi wa kijasiri, ulipokewa kwa shangwe na sherehe na wafuasi wa Raila  si tu wale waliokuwa wamekusanyika nje ya majengo ya Mahakama bali pia  katika ngome zake zikiwamo zile za Kisumu na Kisii.

Mshindi wa nafasi ya Ugavana katika Kaunti ya Kisumu, Peter Anyang’ Nyong’o ambaye ni baba mzazi wa nyota wa filamu za Hollywood, Lupita Nyong’o, ndiye alikuwa akiongoza maandamano ya kusherehekea ushindi huo katika eneo hilo.

Hukumu hiyo imeelezwa na wachambuzi mbalimbali kama ni  ushindi mkubwa kwa Mgombea wa Nasa,  Raila  na mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, ambaye aliishutumu IEBC kwa wizi wa kura ili kumsaidia Kenyatta kushinda tena urais.

Uchaguzi mpya wa urais wa Kenya unatakiwa kufanyika kabla ya Oktoba 31 mwaka huu, huku Tume ya Uchaguzi  ikiamriwa kuandaa uchaguzi mpya bila kuchelewa kama sheria inavyotaka na zaidi kuuendesha kwa uwazi  na kwa mujibu wa sheria.

MSINGI WA KESI

Kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 16, mwaka huu, Katiba ya Kenya inaagiza pingamizi dhidi ya matokeo ya urais linapaswa kutolewa hukumu ndani ya siku 14. Misingi mikubwa ya kesi hiyo ilikuwa kama ifuatavyo:-

Mosi, kuangalia iwapo uchaguzi mkuu wa 2017 uliandaliwa kwa kufuata katiba na sheria za uchaguzi.

Pili, kuangalia iwapo kulifanyika udanganyifu na makosa yoyote.

Tatu, kuangalia iwapo kulikuwa na udanganyifu na je, udanganyifu huo uliathiri vipi uchaguzi.

Nne, Mahakama ya Rufaa inalo jukumu gani kutoa kulingana na kesi iliyofunguliwa.

HOJA ZA ODINGA

Mosi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, IEBC, Wafula Chebukati, alitangaza matokeo ya mwisho ya urais bila kujumuisha kura 11,000 za namba 43A kwa kuwa zilizowasilishwa za 34B zilikuwa za kughushi.

Pili, uchaguzi haukuendeshwa kwa misingi ya haki kama katiba na sheria za uchaguzi inavyotaka ikiwa ni pamoja na mawakala wa vyama vya siasa kuweka sahihi katika fomu za matokeo.

Tatu, Rais Kenyatta alivuruga uchaguzi kwa kuwatishia maofisa wa utumishi wa umma na makatibu wa mawaziri akiwataka wamfanyie kampeni.

Nne, Tume ya Uchaguzi, IEBC haikutumia taarifa rasmi katika vituo vya uchaguzi na maofisa wake wakati wa uchaguzi.

Tano, IEBC haikutumia ibara ya 10 ya sheria ya mwaka 2017 ya matumizi ya teknolojia, hususani walipoulizwa kama uchaguzi huo utakuwa wa kielektroniki zaidi.

UTETEZI WA UHURU KENYATTA

Mosi, IEBC ilifuata sheria na kutumia fomu namba 34B kutangaza mshindi wa uchaguzi, kwa hiyo pingamizi halikuwa na idadi ya kura kupinga zile zilizotangazwa na tume.

Pili, mawakala wote walisaini fomu na hakuna ushahidi unaothibitisha zilighushiwa kama inavyodaiwa na walalamikaji (Nasa) na uchaguzi ulifuata misingi ya Katiba na kuheshimu maamuzi ya wapigakura.

Tatu, maofisa wa Kenyatta hawajihusishi na kampeni za uchaguzi kwa kuwa wao ni watumishi wa umma. Hivyo hawakuwa tishio. Makatibu wa baraza la mawaziri wanateuliwa kwa misingi ya kisiasa na si sheria na kanuni za utumishi wa umma, hivyo wanaruhusiwa kushiriki kampeni za uchaguzi mkuu.

Nne, matumizi ya teknolojia yanalenga kusaidia mfumo uliopo wa kuhesabu kura kwa hiyo madai yaliyomo kwenye pingamizi ni ya kusadikika.

HUKUMU YA MAHAKAMA

“Uchaguzi si tukio bali ni mchakato. Baada ya kupitia ushahidi wote uliowasilishwa, tumeridhishwa kwamba uchaguzi haukuendeshwa kwa misingi  ya Kikatiba na kanuni zake. Jopo la Majaji limebaini kuwa Uhuru Kenyatta hakutangazwa kihalali kama mshindi wa uchaguzi wa Agosti 8,” alisema Jaji Mkuu David Maraga.

Baada ya kutangazwa hukumu hiyo, wakili aliyekuwa akimwakilisha Kenyatta kortini, Ahmednasir Abdullahi na wale wa IEBC, walipinga hukumu hiyo na kutaka maelezo yanayothibitisha hatua hiyo.

Wakili Abdullahi alidai uamuzi wa mahakama ulikuwa na harufu ya kisiasa kwa sababu hakuna mpigakura aliyeshinikizwa kufanya uamuzi wa kuwachagua wagombea wa urais.

Aidha, alibainisha kuwa jopo la majaji limepingana na matakwa ya Wakenya. Hata hivyo, Jaji Maraga, alisema katika muda mwafaka watasema kwanini walifikia uamuzi huo.

Kwa upande wa wanasheria wa Nasa wakiongozwa na James Orengo, walifurahishwa na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa na kuishukuru kwa kukubaliana nao kwamba IEBC ilivurunda.

“Hii ni hukumu ya kwanza katika Bara la Afrika ambayo imefuta matokeo ya uchaguzi mkuu. Mahakama imewapa Wakenya kitu cha kujivunia baada ya kusimamia misingi ya Katiba ya Kenya.

Kwa upande wake Raila alisema amepokea vyema uamuzi wa majaji na kupendekeza tume ya uchaguzi nchini Kenya ishtakiwe.

“Heshima ya Mahakama Kuu sasa imerudi. Nafurahi kuwa Mkenya leo. Lazima tuchunguze kwa makini mwenendo wa IEBC. Hatuna hakika kama itaendesha uchaguzi huru na wa haki,” alisema Odinga.

 KAULI YA KENYATTA

Kwa upande wake, Kenyatta alisema hakubaliani na hukumu iliyotolewa na majaji sita wa Mahakama ya Rufaa kufuta matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi na kutetea kiti chake.

Hata hivyo, alibainisha kuwa anaheshimu pingamizi la Odinga dhidi ya ushindi wake wa urais.

Lakini amewaomba Wakenya kulinda amani na kuachana na misingi ya ukabila haraka iwezekanavyo.

Akizungumza katika hotuba yake kwa umma, Kenyatta alisema anaamini chama chake cha Jubilee kitashinda tena uchaguzi ujao.

Amewaomba wanasiasa wa vyama vya upinzani kufanya kampeni kwa amani na kusisitiza kuwa pande zote mbili zinazochuana kwenye uchaguzi si maadui wala hawapo vitani.

KAULI YA TUME YA UCHAGUZI

Mara baada ya kutolewa hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Wafula Chebukati, naye alizungumza na waandishi wa habari akisema hana mpango wa kujiuzulu nafasi yake.

Chebukati amesema hayo na kusisitiza kuwa atamwomba Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Keriako Tobiko, kufanya uchunguzi iwapo kulikuwa na namna yoyote ya watu binafsi kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi kama hukumu ya Mahakama ya rufaa inavyosema.

Zaidi alisema bodi ya uchaguzi itafanya mabadiliko ya ndani kabla ya zoezi la uchaguzi mpya kuanza na taarifa zitatolewa kwa umma.

GHARAMA ZA UCHAGUZI KENYA

Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 8, mwaka huu unatajwa kuwa wa gharama kubwa ambapo kiasi cha dola za Kimarekani bilioni moja zimetumika.

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Qaurtz Africa, Tume ya Uchaguzi, IEBC inatumia kiasi cha shilingi za Kenya bilioni 43 sawa na Dola za Kimarekani milioni 413.2 kugharamia masuala ya kiufundi, vifaa, elimu kwa wapigakura, kukusanya matokeo na kutuma matokeo.

Aidha, kiasi cha shilingi bilioni nne zilitumika katika masuala ya ulinzi na usalama, kulinda mipaka, kuchapisha vitambulisho vya kitaifa pamoja na masuala ya mahakama na idara ya usalama na ulinzi kwa rais, ambazo zinaingia moja kwa moja au kupitia mambo mengine.

Matumizi ya fedha kwa upande wa Serikali na taasisi binafsi zote ziko juu kuliko wakati wowote katika historia za chaguzi katika nchi hiyo.

Kwa upande wa wagombea katika nafasi mbalimbali, mamia ya mamilioni ya Dola za Kimarekani zinaelezwa kutumika katika ngazi mbalimbali.

Mwaka 2013 zoezi la Uchaguzi Mkuu nchini Kenya liligharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania trilioni 20.

Kenya ni nchi inayoongoza kutumia gharama kubwa katika uchaguzi barani Afrika, ikifuatiwa na Ghana, Tanzania, Uganda na Rwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles