32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

HEROIN NI ZAIDI YA STAREHE ZOTE DUNIANI

Na HAMISA MAGANGA,

TATIZO la matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa duniani kote. Watu wengi wameathirika; wanaume, wanawake, watoto, wazee na vijana wameangamia kwa kuendekeza kilevi hiki.

Miongoni mwa dawa za kulevya ambazo watu huzitumia ni Heroin.

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo cha Madaktari Muhimbili (MUHAS), Fileuka Ngakongwa, anaeleza kuwa Heroin ni jamii ya dawa katika kundi la Opioids.

Dk. Ngakongwa anasema aina hii ya dawa za kulevya imetengenezwa kutokana na dawa nyingine aina ya Morphine inayovunwa kutoka mbegu za mimea inayoitwa poppy plant, inayopatikana nchi za Asia.

Anasema kuwa wataalamu walitengeneza dawa hizi kwa lengo la kutuliza maumivu (analgesic).

“Heroin yenyewe ilitengenezwa kwa dhumuni la kutibu kifua kikuu… zina uwezo wa kuondoa maumivu makali kwa kuzuia ubongo kupokea taarifa kutoka sehemu ya mwili inayouma.
“Hospitali nyingi hutumia Morphine, Pethidine ambazo hutengenezwa kikemikali na Codeine kwa kutuliza maumivu hasa kwa wagonjwa wa saratani, waliofanyiwa upasuaji na wale wenye maumivu makali yaliyotokana na ajali,” anasema Dk. Ngakongwa.

Kwa kawaida Heroin huonekana kama unga mweupe, kijivu au kama nta nyeusi kwa namna ilivyoandaliwa.

Inasemekana kuwa Heroin iliwahi kutumika kutibu wanajeshi wa Marekani waliokuwa na magonjwa ya msongo wa mawazo (Post Traumatic Stress Disorder), iliyosababishwa na kumbukumbu za matukio ya kutisha waliyoshuhudia vitani – Vietnam.

Magonjwa haya huambatana na ndoto za kutisha na hata kuyaona upya matukio yale yaliyopita (visual hallucinations).

Dk. Ngakongwa anasema kuwa Heroin inaweza kumfanya mtu kusikia raha.

Anasema hii ni kwa sababu hustua seli za ubongo kuzalisha homoni aina ya Dopamine ambayo humfanya mtu kusikia raha.

Homoni hii hutolewa kwa kiasi cha uniti 1,200 – 1,800 baada ya kutumia Heroin kulinganisha na uniti 150 – 200 tu zitolewazo wakati mtu anaposhiriki ngono.

Hivyo basi, Heroin huleta raha karibu mara tisa ya ile itokanayo na ngono, tena kwa muda wa takribani dakika 30 – 45.

“Hizi dawa huwa zinatolewa kwa uangalifu wa hali ya juu kwa sababu kuna watu huzitumia kama kilevi.

“Katika mwili wa binadamu, kuna kiwango cha wastani cha Opioids (Endogenous Opioids) ikiwa na kazi mbalimbali, lakini kubwa zaidi ni kutuliza maumivu… huwa zinafanya kazi katika ‘receptors’ ziitwazo mu, kappa and delta.

“Hizi receptor zinapatikana kwa wingi kwenye ubongo na uti wa mgongo,” anasema daktari huyo.

Anasema licha ya kazi hiyo, pia zinachangia kuhamasisha kazi nyingine kama kukufanya usikie utamu wa chakula, hisia na kuhisi raha wakati wa tendo la ndoa.

Dk. Ngakongwa anasema kuwa mbali na kuhamasisha, wakati mwingine huwa zinaondoa ama kupunguza raha hizo.

Anasema Heroin na Dopamine hufanya kazi pia katika mfumo wa ubongo, ambapo huchochea vitu vingi kama ngono, chakula, muziki… vitu vyote ambavyo humpa mwanadamu raha.

“Hali hiyo huwa inaamshwa na Dopamine… kwahiyo, Dopamine zikiwa nyingi raha nayo huzidi.

“Kazi ya Heroin na Opioids nyingine huwa zinapunguza kemikali iitwayo Gaba, ambayo huzuia kazi za Dopamine katika mfumo huo.

“Kwahiyo, Heroin inaweza kukupa starehe kama ile unayopata pindi unapofanya ngono, kucheza muziki, kula chakula kizuri au kunywa pombe,” anasema Dk. Ngakongwa.

Anasema kwa sababu hii, mtumiaji wa kilevi hiki kwa starehe anayoipata anaweza asione haja ya kutafuta starehe nyingine kwa kuwa Heroin inakuja kikamilifu na kwamba haifanyi kazi sehemu moja tu katika ubongo.

Wataalamu wa masuala ya dawa za kulevya wanasema kuwa Heroin hufanya akili ya mtumiaji kupumbaa na hivyo kuhitaji kiasi kikubwa zaidi kwa mara nyingine.

Seli za ubongo huongeza vipokezi vya homoni ya Dopamine ili kupokea homoni nyingi inayozalishwa, hali ambayo husababisha ubongo kuhitaji Heroin zaidi ili kukidhi haja.

Arosto
Wakati Heroin inapoisha mwilini, mwili hutamani zaidi. Hapo ndipo hutokea ‘arosto’, ambapo mtumiaji hutaabika kwa kukosa raha isiyo kifani, maumivu makali ya tumbo, viungo na kichwa. Kuhisi baridi kali, mapigo ya moyo kwenda kasi, mwili kutetemeka, kujisikia vibaya, kuchoka, kushindwa kula na dalili nyingine mbaya. Hali hiyo ndiyo humfanya mtumiaji kutafuta namna ya kuipata Heroin haraka iwezekanavyo iwe kwa njia halali au haramu.

Utegemezi
Matumizi zaidi ya Heroin huzaa arosto sugu na kusababisha kuwa tegemezi kwa dawa hizo. Mtumiaji hushindwa kufanya shughuli yoyote bila kutumia Heroin.

Madhara
Dk. Ngakongwa anasema madhara ya matumizi ya Heroin ni makubwa na hatari.
Anayataja madhara hayo kuwa ni kuhisi kichefuchefu, kutapika, kuwashwa, kuchoka, kukosa nguvu na akili kushindwa kufanya kazi kwa ufasaha.

Madhara mengine ni mishipa ya damu kuweza kusinyaa na kushindwa kusafirisha damu kwa kiwango kinachotakiwa, makovu na upele wa ngozi unaosababishwa na kujidunga, mirija ya moyo huweza kuharibiwa, magonjwa ya mapafu, udhaifu wa misuli, kukosa usingizi, kinga ya mwili kupungua na hivyo kurahisisha magonjwa ya maambukizi, kupoteza uwezo wa kushiriki tendo la ndoa, kupoteza uwezo wa kuzaa (ugumba na utasa), mfadhaiko, Ukimwi, homa ya ini, kupoteza fahamu na hatimaye kifo.

Madhara ya matumizi ya muda mrefu wa dawa hii hutokana zaidi na matumizi ya sindano na vifaa vingine visivyo salama.

Jinsi Heroin inavyotumiwa

Aina hii ya dawa ya kulevya huweza kutumika kwa kuvuta kupitia pua, kuvuta kama sigara au kujidunga kwenye mshipa kupitia sindano.

Siku hizi watu hutumia njia ya haja kubwa na kwenye uke, ambapo kuta hufyonza Heroin na kuanza kufanya kazi ndani ya sekunde 40.

Dk. Ngakongwa anasema kuwa Heroin mara tu baada ya kuingia kwenye damu, huenda kwenye mfumo wa neva na kukandamiza ufanyaji kazi wake, hapo ndio huweza kutumika kupunguza maumivu.

Dalili za mtu aliyetumia Heroin
Mara mtu anapotumia Heroin huanza kujisikia mwenye furaha na raha na kuhisi usingizi.

Dalili nyingine ni midomo kuwa mikavu, misuli kuishiwa nguvu, kuhema taratibu, mikono na miguu kuwa mizito na kope za macho kulegea.

Dk. Ngakongwa anasema mtu anayetumia Heroin si tu  anadhoofisha kinga ya mwili, bali pia anajiweka katika tabia hatarishi ya matumizi ya kujidunga sindano na kufanya ngono isiyo salama. Mchanganyiko huu wa tabia ndio ambao huongeza mara dufu hatari ya kuambukizwa Ukimwi na magonjwa mengine mengi.

Madhara kwa wajawazito

Matumizi ya Heroin kwa mjamzito husababisha mtoto na mama kuwa tegemezi kwa dawa hiyo kwa kuwa humfikia mtoto aliye tumboni kupitia placenta.

Dalili kwa mtoto aliyeathirika

Mtoto ambaye mama yake alitumia dawa za kulevya alipokuwa tumboni, mara nyingi huwa analia sana, anapata homa, anakakamaa kama mtu mwenye kifafa, anaongezeka uzito taratibu, anahara, anatetemeka na wakati mwingine hupoteza maisha.

Watoto hawa huhitaji kulazwa hospitali kwa uangalizi wa karibu na kupewa matibabu ya dawa kama Morphine ili kutibu dalili hizo.

Matibabu

Matibabu ya Heroin yamegawanyika katika makundi makuu mawili – kumpatia mtumiaji ushauri nasaha ili kumsaidia abadili tabia na pili ni matumizi ya dawa ambazo hutibu dalili za ugonjwa na kumwezesha kuachana na matumizi ya dawa hii hatari. Mfano wa dawa hizi ni kama Morphine, Methadone, Naltrexone na Buprenorphine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles