25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NANCY SUMARI NA MKAKATI WA KUWAJENGA WATOTO, VIJANA

Na MWANDISHI WETU,

NANCY Sumari si jina geni nchini Tanzania. Tangu mwaka 2005 aliposhinda tuzo ya kuwa mrembo wa Tanzania na kuwa mshindi wa Miss World Africa  amekuwa ni simulizi ya kuvutia.

Akiwa na uzoefu wa kuwa mjasiriamali wa ukweli – Mkurugenzi Mtendaji wa  Kundi la Bongo5 Media na hali kadhalika Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Neghesti Sumari na Jenga Hub.

Hamasa iliyotokana na Jenga Hub ni kutaka kutatua changamoto zilizopo  ndani ya jamii.

Wiki iliyopita  Tigo Tanzania kwa kushirikiana na asasi isiyo ya kiserikali ya Reach for Change,  ilimpatia tuzo ya Dola za Marekani 20,000 baada ya kuwa mshindi mwenza wa  shindano linaloitwa Waleta Mabadiliko Kidijitali wa Tigo akitoka miongoni mwa washiriki 350. Mshindi mwingine ni Sophia Mbega  ambaye aliwavutia majaji kwa  ubunifu mkubwa wa kidijitali  ambao ulijielekeza katika  kusaidia  makundi ya wanawake  kujisaidia wenyewe  katika mpango unaoitwa Benki za Jumuia Vijijini (VICOBA).

Jenga kama lilivyo neno lenyewe  ambalo Nancy amelitumia  kuunda ubunifu wake wa Jenga Hub, unalenga  kuwapatia watoto na vijana  fursa za kuwa wataalamu wa kidijitali. Wanapatiwa  nafasi ya  kuandaa, kuunda na kuchanua  kupitia teknolojia za  kidijitali. Ubunifu huo unaangalia uwiano uliopo kati ya muundo na uhuru katika kujifunza  kupitia mchakato wa teknolojia.

“Ninafurahi kushinda  tuzo hii; nitahakikisha natumia fedha hizi  vizuri  kuendeleza  maudhui yangu  ili kuweza kuwasaidia watoto  kuzifikia ndoto zao za baadaye,” anasema Nancy na kuongeza;

“Naishukuru mno Tigo na Reach for Change kwa kuanzisha wazo hili zuri ambalo hadi sasa limezaa matokeo chanya kwa jamii.”

Akielezea jinsi ubunifu wake wa Jenga Hub unavyofanya kazi, Nancy anasema  inawapatia watoto fursa sahihi ya kujifunza program za kompyuta, stadi za kiroboti na kuweka alama. Ubunifu huo pia unawawekea wazi watoto misingi ya kujifunza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama vile stadi za program  ambazo zinaweza kugeuzwa na kutumika katika malengo  mapana ya  kielimu na burudani.

 Watakaojiunga watawezeshwa kutumia zana zinazokuwapo katika kompyuta kuanzisha kazi za sanaa, kuchora picha, kuigiza, kuanzisha mtandao wa wavuti, kufanya sanaa za kiroboti, kutunga muziki, uwasilishaji kupitia zana kadhaa habari na mengineyo.

 “Jenga Hub inatoa miundo ya kozi, stadi za kompyuta na matumizi mengine ya msingi,” anasema.

Shindano la Waleta Mabadiliko

Shindano hilo linalenga kutambua na kusaidia wajasirimali jamii ambao wanatumia  zana na teknolojia za kidijitali kuboresha na kuleta mabadiliko  ndani ya jamii pamoja na kizazi kijacho.

Mbali na msaada huo wa kifedha, washindi wamepewa  nafasi ya kuitumia Reach for Change ambayo hutoa ushauri, utaalamu na namna ya kufikia  mitandao mingine duniani ambayo inawawezesha  kujenga  ujasirimali  endelevu wa kifedha  ambao unaleta mabadiliko makubwa na ya kudumu.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez   Waleta Mabadiliko  ambao tayari wako ndani ya program hiyo  wameyagusa  maisha ya watoto zaidi  250,000 nchini Tanzania.

“Tunaamini kwamba kwa nyongeza hii ya waleta mabadiliko  tutaleta mabadiliko  katika maisha ya watoto wengi zaidi na kusaidia kuifanya Tanzania  kuwa sehemu nzuri kwa  vizazi vijavyo,” anasema Gutierrez wakati wa hafla ya kutoa tuzo hizo jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa  mwezi huu.  

Gutierrez aliendelea kufafanua kwamba  kama nembo ya maisha ya kidijitali Tigo inatoa msukumo kwa mawazo na miradi inayoendeshwa  na teknolojia  ambayo yanaleta mabadiliko endelevu.

“Teknolojia ya kidijitali si tu inabadilisha namna ambavyo tunafanya  biashara ndani ya Afrika, bali pia  inaleta mapinduzi  kwa njia tofauti  na  kutatua masuala ya maendeleo ya jamii.

“Hivyo, kutokana na heshima hii kubwa  ni kwamba kwa mara nyingine  tunaunda fursa  kwa  mawazo hayo kutambuliwa, kuungwa mkono na kubadilisha hadi kiwango cha juu cha matokeo ya kijamii na kiuchumi,”anasema.

Huu ni mwaka wa tano ambapo Tigo na Reach for Change  wanatangaza washindi wa shindano hilo. Washindi wanaoingia fainali ambao huchaguliwa kutoka kundi la mamia ya wajasirimali jamii  ambao wametumia zana za na teknolojia kupata suluhisho  kwa matatizo yanayoikabilia jamii ya Watanzania.

Gutierrez aliwapongeza washindi waliotangulia na papo hapo akitoa msukumo kwa wengine  kushirikiana mawazo yao.

 “Mkusanyiko wetu katika ujasiriamali jamii unavutia mno. Hadi sasa tumeshasaidia Waleta Mabadiliko ya Kidijitali nchini Tanzania na tunatarajia kuwasaidia wajasiriamali jamii wengi zaidi kila mwaka ili kusukuma mkakati wetu mbele,” anafafanua Meneja huyo.

Anasema; “tumekuwa msaada mkubwa kwa kazi zote za Waleta Mabadiliko wetu na mwaka huu tunatarajia kuangalia namna ya  kusaidia mashujaa wawili zaidi  na wajasiriamali  jamii walio wabunifu.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles