KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez, amemtaja mchezaji wa zamani wa timu ya Arsenal, Thierry Henry, kuwa msaidizi wake katika benchi la ufundi la timu hiyo.
Henry anaweza kuchukua majukumu hayo ya ukocha baada ya kujifunza akiwa katika timu ya vijana ya Arsenal.
Mkongwe huyo aliifundisha timu ya vijana ya chini ya umri wa miaka 18 ya Arsenal kabla ya kulazimika kuondoka baada ya Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, kuamuru kufanya hivyo kutokana na kitendo chake cha kuendelea na uchumbuzi katika televisheni ya Sky Sport.
Hata hivyo, Henry ataruhusiwa kuendelea na kazi yake ya uchambuzi wakati wa mapumziko, licha ya kuteuliwa kuifundisha timu hiyo.
Mkongwe huyo ataungana na Martinez na kocha msaidizi, Graeme Jones, katika benchi la ufundi la timu hiyo.
Katika kutekeleza majukumu yake, Henry anatarajia kuwafundisha wachezaji kama Eden Hazard, Morouane Fellaini na Kevin De Bruyne.