Na JANETH MUSHI- KARATU
HEKARI zaidi ya 200 za mahindi na vitunguu katika Kijiji cha Kangdet, zimekauka kwa kukosa maji.
Hali hiyo imetokea baada ya Serikali kuagiza mashine za kuvuta maji zinazodaiwa kuwekwa kwenye vyanzo vya maji pamoja na mto ziondolewe.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kijiji hicho kilichopo Tarafa ya Eyasi, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, wamelalamikia hatua hiyo ya Serikali kwa kile walichosema kuwa itasababisha kuyumba kwa uchumi wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mashamba hayo yaliyoathirika pamoja na kwenye mkutano mkuu wa kijiji hicho, wananchi hao walisema wamekuwa wakitumia vyanzo hivyo vya maji kwa muda mrefu katika kilimo cha umwagiliaji.
Mmoja wa wakulima hao, Halima Hamisi, alisema hawana tegemeo jingine zaidi ya kilimo hicho cha umwagiliaji, Serikali inatakiwa kuruhusu mashine hizo za umwagiliaji kabla maisha yao hayajawa mabaya zaidi.
“Mazao yamekauka kutokana na agizo hilo la Serikali wakati sisi tunategemea kilimo kwa chakula na biashara.
“Siku zote tumekuwa tukitunza vyanzo hivyo kwa miaka yote na kila mwezi tumekuwa tukitoa fedha kwa ajili ya mgambo wanaolinda eneo hili ambalo ni kame kwa asili,” alisema Halima.
Akizungumza na wananchi hao, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Haruna Kassim, alikiri mazao hayo kukauka na kwamba tayari wameshatoa taarifa wilayani juu ya hali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo, alisema mashine ziliondolewa maeneo zilikokuwa kutokana na maombi ya wananchi.
“Wananchi ndio waliosema tuondoe mashine hizo, sasa tumeziondoa wanaanza kulalamika, hii si sawa kabisa,” alisema Mahongo.