Na GLORY MLAY
MZUNGUKO wa pili wa Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), umepangwa kuendelea leo kwa michezo saba kupigwa katika Viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.
Mchezo wa kwanza utakaofungua dimba utazikutanisha timu ya Kigamboni ambayo itatoana jasho na JKT.
JKT itaivaa Kigamboni ikiwa na rekodi ya kucheza michezo 21 na kupoteza miwili pekee, matokeo yaliyoiweka kileleni mwa msimamo wa RBA, baada ya kuvuna pointi 40.
Kwa upande wa Kigamboni, wao wameshuka dimbani mara 20 hadi sasa, wameshinda michezo miwili na kupoteza 18.
Matokeo hayo yameifanya kufikisha pointi 22 na kukalia nafasi ya 14.
Michezo mingine itakayochezwa leo ni Udsm Insider dhidi ya Pazi, wakati timu ya DB Liones itapepetana na Ukonga Queens, mchezo utakaozikutanisha timu za wanwake.
Pazi watakutana na wapinzani wao wakiwa na rekodi ya kucheza michezo 19 na kupoteza mitano, hatua iliyoiweka nafasi ya sita, baada ya kuvuna pointi 32.
Udsm Insider kwa upande wake, imecheza michezo 19, ikishinda minne na kupoteza 15.
Matokeo hayo yameifanya kufikisha pointi 23 na kukalia nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hiyo.
Nayo Oilers itashuka dimbani kuikabili Magnet, Â Kurasini itapepetana na Vijana, DB Liones itakamuana na Tanzania Prisons na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya ABC na Mabibo Bullet.