KULWA MZEEÂ -DAR ES SALAAM
VIGOGO wanaotuhumiwa kwa uhujumu uchumi wamekuwa wakitoka kwa msamaha, lakini macho ya Watanzania na masikio yanasubiri kuona kama mabosi wa IPTL, Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira kama leo watatoka ama la.
Washtakwa hao leo wanatarajiwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuhudhuria kesi yao inayotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Sethi anadaiwa kuandika barua ya msamaha na kukiri makosa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwa mujibu wa sheria mshtakiwa akifanya hivyo anafikishwa mahakamani kukamilisha taratibu za kisheria, ikiwemo makubaliano waliyoingia kusajiliwa rasmi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Rugemalira hakuandika barua kwa sababu anazoona ni za msingi.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
MCHINA
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru raia wawili wa China, Li Ling na Chen Guo, baada ya kukiri makosa ya uhujumu uchumi na kulipa fidia ya Sh milioni 70.
Mahakama imekubali maombi ya Jamhuri na kutaifisha gari aina ya Toyota Prado T 982 CDH na mashine mbili za washtakiwa hao na kuwa mali ya Serikali, huku ikimtaka Guo kulipa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kuishi nchini bila kibali.
Upande wa mashtaka umewafutia washtakiwa hao mashtaka ya kutakatisha fedha na kuwasomea mashtaka mawili ya kujihusisha na nyara za Serikali na kuishi nchini bila kibali.
Washtakiwa wengine wanne waliokuwa katika kesi moja na raia hao wa China wamegoma kukiri mashtaka yao hivyo kurudishwa rumande.
Akisoma adhabu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema Li Ling atatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni 45 na Guo atalipa Sh milioni 25 na faini ya Sh milioni moja au kwenda jela mwaka mmoja.
Alisema pia gari aina ya Toyota Prado na mashine mbili zinataifishwa na kuwa mali ya Serikali na amewataka washtakiwa hao kuondoka nchini mara moja kwa kuwa si raia wa Tanzania.
Wakili Salimu Msemo alidai kuwa wameingia makubaliano na washtakiwa hao baada ya kukiri kosa la kujihusisha na nyara za Serikali na kuishi nchini bila kibali, hivyo wameamua kuondoa mashtaka ya kutakatisha fedha.
Baada ya kusoma makubaliano hayo, Hakimu Shaidi aliwaapisha washtakiwa na kuwauliza kama walisaini kwa hiari yao na kudai walifanya hivyo kwa hiari yao.
Akisoma mashtaka mapya, Wakili Msemo alidai Julai 5, 2015 katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mshtakiwa Li Ling Ling alisafirisha nje ya nchi kucha 25 za simba zenye thamani ya Sh 22, 500,000 bila kuwa na kibali.
Alidai katika kosa jingine Julai 5, 2015 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mshtakiwa Cheng Guo alisafirisha nje ya nchi meno 21 ya simba yenye thamani ya Sh. 12, 500,000 bila ya kuwa na kibali.
Msemo katika shtaka jingine alidai Januari 18, 2015 Chen Guo alikutwa akiwepo nchini kinyume na sheria.
MPEMBA WA MAGUFULI
Mfanyabiashara Yusuf Ali maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli’ na wenzake nao wameandika barua kwa DPP kuomba msamaha kwa makosa ya kufanya biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6 bila kibali.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kwamba Jamhuri wamepokea barua kutoka kwa washtakiwa kwamba wanataka kukiri makosa yao.
Mkunde aliomba muda wa kufanya mawasiliano na washtakwa ili kukamilisha mchakato huo. Mahakama ilikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Oktoba 16.
Mbali ya Mpemba, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande vya meno ya tembo 50 vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia inadaiwa Oktoba 26, mwaka huu, washtakiwa hao wakiwa Mbagala Zakhem, Dar es Salaam walikutwa na vipande vya meno ya tembo 10 vyenye uzito wa kilo 13.85 vya thamani ya Dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.
Wanadaiwa kuwa Oktoba 27, mwaka huu, wakiwa Tabata Kisukuru washitakiwa hao walikutwa na vipande vinne vya meno hayo ya tembo yenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya Dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni 32.7 .
Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.