NA CHRISTOPHER MSEKENA
FAMILIA ya Hip hop na mashabiki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, hivi karibuni waliadhimisha miaka sita ya kifo cha rapa Langa Kileo, aliyefariki dunia Juni 13, 2013 katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Jambo linaloweza kushangaza wengi ni vile ambavyo kumbukizi hii ya kifo cha Langa, inavyopewa uzito mkubwa na kila anayehusika kwenye tasnia ya burudani hata wale ambao hawakuwahi kuupenda muziki wa Hip Hop.
Kuna sababu nyingi ambazo zinafanya Langa, akumbukwe kiasi hicho. Utu, ucheshi na uwezo wake wa kutunga muziki unaogusa jamii moja kwa moja ndiyo sababu kubwa ya kufanya akumbukwe kila inapofika Juni 13.
Ukiacha hayo, kuna jambo muhimu ambalo Langa alilifanya kwa ufanisi mkubwa na kuacha alama ya kipekee kwenye muziki wa Hip hop ukiacha nyimbo zake kali Rafiki wa Kweli, Kifo Jela au Taasisi, Matawi ya Juu, Gangstar, Swaingilish, Pipi ya Kijiti na nyinginezo.
Alikuwa ni msanii anayetoa elimu juu ya dawa za kulevya. Kama tunavyojua kuwa Langa alikuwa miongoni mwa wasanii waliokiri kuathirika na dawa za kulevya hivyo alitumia nafasi yake kama msanii kutoa elimu kwa jamii.
Kupitia wimbo Kifo, Jela au Taasisi, Langa alibainisha vyema namna ambavyo dawa za kulevya zinamaliza nguvu kazi ya Taifa. Aliweka wazi kuwa mtumiaji yeyote wa dawa za kulevya mwisho wake lazima uangukie kwenye majanga matatu.
Kama siyo kifo kutokana na utumiaji wa dawa hizo basi mtumiaji wa dawa za kuleva ataishia kwenda jala kutokana na matukio ya kiharifu ambayo atayafanya pindi atakapotumia dawa hizo au atakapotaka kupata pesa kwannjia isiyo halali ili akavute unga.
Au mtumiaji wa dawa za kuleva anaweza kuishia kwenye taasisi za kutibu warahibu. Hivyo ndivyo ambavyo Langa alijipambanua vyema kama msanii wa Hip Hop anayepinga dawa za kulevya yeye akiwa shuhuda.
Tunapo adhimisha miaka sita ya kifo chake tunapaswa kutafakari namna ya kuendeleza harakati zake kwani tatizo la dawa za kulevya balo lipo na linahitaji sanaa ili kufikisha ujumbe kwa jamii kujiepusha na janga hilo.