Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mkonge ni moja kati ya zao la biashara Tanzania,asili ya zao hili ni Mexico na baadae likasambaa katika nchi za India na Tanzania mwaka 1892.
Inaelezwa kuwa zao la Mkonge liliingizwa nchini na mtaalamu wa kijerumani Dr.Richard Hindorff ambaye alikua mtafiti wa mimea na udongo.
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyopo sasa, zao hili linaweza kuwa mbadala kwa maeneo ya vijijini kwani zao la Mkonge lina sifa za kustahimili hata kwenye maeneo ambayo mazao mengine hayawezi kustawi.
Mwaka 2019 Serikali ilitangaza zao la mkonge kuwa moja kati ya mazao saba ya kimkakati hapa nchini.
Kutokana na hilo Serikali imeiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kwa kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa uzalishaji wa zao la mkonge unaongezeka kutoka tani 36,000 mwaka 2019 kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.
Mkakati huo pia unahusisha maeneo mbalimbali ikiwamo kuhamasisha na kushirikisha wakulima wadogo na upatikanaji wa masoko.
Mahitaji makubwa ya mkonge kwa sasa ni kuzalisha bidhaa mpya kama vile composite kwa ajili ya viwanda vya magari na shughuli za ujenzi, Sukari, pombe kali, karatasi maalum.
Nchi ambazo ni wanunuzi wakuu ni China, Saudi Arabia, Nigeria, India, Uhispania, Ujerumani, Moroko, Japani ,Kenya na Israel.
Happiness Nyitu ni mmoja wa Watanzania walioona fursa katika zao la mkonge ambapo kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Sisal Fibre L.t.d inayohusika na uuzaji wa nyuzi za mkonge.
Mfanyabiashara huyo anasema alianzisha kampuni mwaka 2020, ambapo tayari inafanya viziri katika kuuza bidhaa za mkonge ndani na nje ya nchi.
Anasema kwa sasa soko lake lipo barani Asia, Ulaya na Afrika, huki akitarajia kufungua kampuni nyingine Afrika Magharibi mwanzoni wa mwaka 2024.
“Tuna kiwanda kidogo cha kuchakata mkonge katika level za kuuza ndani na nje ya nchi tunanunua mkonge sehemu mbalimbali za mikoa nchini ikiwemo Manyara, Mara, Simiyu, Shinyanga, Singida, Morogoro, Dodoma, Tanga na mikoa mingine inayozalisha mkonge,”amesema Nyitu.
Amesema wamekuwa wakinunua kwa wakulima wadogo ambao wanakuwa wamechakata nyuzi kwa kiasi baada ya hapo wanapeleka kiwandani kuchakata kwa ngazi za kimataifa .
“Kwa nini niliingia kwenye biashara ya kuuza nyuzi zitokanazo na mkonge? Ni kutokana na historia tuliyonayo ilinifanya nijiulize kwa nini hatuuzi mkonge kama zamani nini kinasababisha?, “amesema.
Amesema alifanya utafiti mdogo na kugundua kwamba nyuzi za plastiki zimechukua sehemu kubwa za mkonge lakini bado zao hilo lina matumizi mengi.
Nyiti anasema wanaendelea kufanya utafiti ili kuweza kutengeneza bidhaa nyingine za mkonge kulingana na ukuaji wa teknolojia.
Anaeleza kiwa nyuzi wanazalisha zinazotumika kutengeneza vifaa vya ujenzi, mbolea, chakula cha mifugo na vitu vingine.
Amesema soko la ndani wanafanya kwa asilimia ndogo kwa sababu wamewaachia wajasiriamali ambao bado mitaji yao ni midogo na hawezi kuuza soko la nje.
Amesema mkonge ni kama dhahabu na kujivunia mafanikio aliyopata kupitia biashara hiyo ikiwamo kupanua soko lake.
“Mafanikio mengine ni ongezeko la uchumi kila anaye shiriki kwenye biashara ya mkonge na nimewapatia ajira vijana na wakina mama, haya ni mafanikio, “amesema.
Akizungumzia kuhusu changamoto zinazowakabili ni kushindwa kufikia masoko kwa urahisi pia uchakataji kwani wanahitaji mashine bora ili kutoa mkonge wenye ubora wa juu.
Changamoto nyingine ni gharama za usafiri zimepanda na upatikanaji wa mikopo ya kilimo kwa wanaojihusisha na uchakataji wa mkonge na biashara.
Aidha Nyiti akizungumzia kongamano la wanawake katika biashara chini ya mkataba wa eneo huru la biashara Afrika(AfCFTA) lililofanyika kwa siku tatu na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi 55 Afrika, jijini Dar es Salaam, anasema anajivunia kwani ameweza kupata cheti cha kumtambua.
Anaeleza kuwa Januari, 2023 alishiriki mkutano ulioandaliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dk.Ashatu Kijaji alieelezea soko huru eneo la biashara na kampuni ambazo zipo tayari kusafirisha mkonge kupitia makubaliano ya soko huru la Afrika.
“Nilimuahidi kuwa nipo tayari kll kusafirisha kupitia soko huru la Afrika, mnamo Agosti mwaka huu nilipata cheti cha uhalisia wa bidhaa kupitia soko huru la Afrika (Certificate living Under AfCFTA) na hiki cheti cha kwanza kupitia mkutano huu,”ameeleza.
Amesema yeye ni mwanamke wa tatu nchini kusafiri bidhaa kwenda soko huru la Afrika na mwanamke wa kwanza kusafirisha mkonge kupitia soko hilo na faida walizopata kuongeza wateja na kuendeleza kutangaza zao la mkonge.
Ameeleza kufanyika kwa kongamano hilo ni chachu ya kuhamasisha wanawake wengine kufanya biashara katika soko hilo,fursa zipo nyingi hivyo wachangamkie.
Nyiti anasema matarajio ambayo wanategemea kupitia kongamano hilo ni masoko mapya na wateja ndani ya bara na ongezeko la matumizi ya mkonge katika ngazi zote na kupanda kwa uchumi Afrika.
“Itasaidia ‘social economic development’ kwa wanawake, mojawapo kwenye kujishughilisha na kazi za mkonge shambani na viwandani na biashara ipo wazi kikubwa kufuata utaratibu na sheria zilizowekwa, “amesema.
Ameongeza kuwa wanawake wanatakiwa kuwa wengi kufanya biashara katika soko hilo kwa sababu ni walengwa wa kwanza na kujiunga katika vikundi kuweza kufanya biashara.
Nyiti ameshauri katika sehemu wanazofanya kazi kuwepo na vitendea kazi kati ya mama na mtoto itawasaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa.
“Kama kinara wa usafirishaji wa bidhaa kwenye soko huru la Afrika naamini watakuja wanawake wengi zaidi na nipo tayari kuwaongoza njia wanawake wenzangu katika soko hili wakati ndo sasa na milango ipo wazi,”amesema.