25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hapi: Vyombo vya ulinzi shughulikieni uvaaji barakoa, unawaji mikono

 GODWIN SIWONIKE -IRINGA 

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo, kufuatilia uvaaji wa barakoa na unawaji wa mikono kwa sabuni na maji tiririka katika vyombo vya usafiri na sehemu za biashara.

Alisema hayo wakati akipokea msaada wa vifaa vya kudhibiti virusi hivyo iliyotolewa na kampuni za Qwihaya General Enterprises na Asas Group.

Vifaa hivyo ni pamoja na mavazi maalumu ya watoa huduma (PPE), vipima joto, vitakasa mikono, sabuni, barakoa na tenki za maji.

Hapi alisema tayari ugonjwa huo umeingia Iringa na akawataka wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kujikinga na virusi hivyo.

Taarifa iliyotolewa na kiongozi huyo inaonesha mtu mmoja aliyetokea Dar es Salaam, alifariki dunia April 19, mwaka huu kutokana na corona.

Aliwapongeza wadau wanaounga mkono mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo kwa kutoa misaada ya vifaa na vifaa tiba. 

Aliwataka wakazi wa mkoa huo kuchukua tahadhari za kujikinga na virusi hivyo ikiwamo kuepuka maeneo yenye msongamano, kunawa mikono kwa maji titirika na sabuni au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia barakoa na kila mtu kukaa angalau mita moja kutoka alipo mwenzake.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa za watu wenye dalili za ugonjwa huo na kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma.

Katika vifaa alivyopokea Hapi, Asas Group imetoa msaada wa mavazi 40, barakoa 1,200 na dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh milioni 9.8.

Taasisi zingine zilizotoa msaada wa vifaa hivyo ni pamoja na SAI Energy ya mjini Iringa iliyotoa katoni 15 za vitakasa mikono zenye thamani ya Sh 750,000 na taasisi ya Clinton iliyotoa vipima joto saba, barakoa 120, mavazi mawili na karatasi 300 za matangazo.

Nyingine ni taasisi ya MOH ya mjini Dodoma iliyotoa vipima joto viwili, barakoa 4,000 za kitiba zinazovaliwa na matabibu wakati wa upasuaji na mavazi maalumu ya watoa huduma 35. 

Kampuni ya Qwihaya General Enterprises ya mkoani Iringa ilikabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 12 kwa mkuu wa mkoa wa Iringa kwa ajili ya kujikinga na virusi vya Corona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles