FRANCIS GODWIN, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa, kuwasaka na kuwabana watu wote wanaojihusisha na biashara ya kukopesha fedha zenye riba kubwa kwa wananchi.
Agizo hilo alilitoa mjini hapa jana wakati wa ziara yake ya kupokea na kutatua migogoro ya ardhi wilayani Mufindi.
Alisema watu hao waliokuwa wakikopesha fedha za riba kwa wananchi wamekuwa ni chanzo kikubwa cha wakazi wa Iringa kupoteza mali zao walizoziwekeza kama dhamana ilhali hawalipi kodi TRA.
“Kwa hiyo madudu yapo mengi na saa nyingine mnatuona tunakuwa wakali ila wapo watu wengine wanaojiita haki za binadamu wamekaa Dar es Salaam katika kiyoyozi wanapiga kelele hawajui huku wananchi wanavyonyanyasika kiasi gani na watu wamepoteza ndugu zao kwa kufa kwa presha kutokana na mali zao kupokonywa na hawa wakopeshaji ila yote haya wao hawayaoni wapo kunilalamikia mimi ninayesaidia wanyonge,” alisema.
Alisema hatawasikiliza wachache wanaotetea unyonyaji na badala yake atawasikiliza wananchi walio wengi.
“Wakati mwingine Serikali inaharibiwa na watendaji ambao wameacha kutimiza wajibu wao wa kuwasikiliza wananchi na kutenda haki, mimi sihitaji kabisa kupendwa na wachache wanaotapeli haki za wananchi, nahitaji kupendwa na wanyonge walio wengi ambao kazi yangu ni kuwasikiliza na kuwasaidia,” alisema.