LIGI ya Mabingwa barani Ulaya inatarajia kuendelea leo kwenye viwanja viwili ambapo dunia itasimama kwa muda, hasa kwa wadau wa soka kupisha michezo hiyo.
Kwenye Uwanja wa Emirates, wenyeji Arsenal watawakaribisha wababe wa nchini Hispania, Barcelona, kwenye uwanja huo ambao unabeba watazamaji 60,432.
Arsenal bado ipo katika ubora wake, huku ikiwa inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi kwa alama 51 sawa na Tottenham, wakati nafasi ya kwanza ikishikwa na Leicester City, yenye alama 53.
Hata hivyo, kocha wa klabu hiyo, Arsene Wenger, amedai kwamba huu ni wakati wake wa kuonesha maajabu kwa kuwafunga wababe hao wa nchini Hispania.
“Hatuwezi kuwa wapumbavu kuupoteza mchezo tukiwa nyumbani, hii ni nafasi yetu ya kuonesha ubora katika mchezo huu wa awali.
“Ninaamini mchezo utakuwa wa ushindani mkubwa, lakini tutakuwa na nafasi ya kushinda bila kujali ubora wao,” alisema Wenger.
Wakati huo Barcelona wanaonekana kuwa katika ubora wa hali ya juu, huku wakiongoza katika Ligi ya Hispania.
Kwa upande wa Uwanja wa Juventus, napo nyasi zitatimua vumbi katika mchezo dhidi ya wababe wa nchini Ujerumani, Bayern Munich, ambapo mchezo huu unaonekana kuwa mgumu zaidi kutokana na ubora wa timu zote.
Katika mchezo huu tutashuhudia ufundi wa hali ya juu kwa timu zote na kunaweza kukawa na mashambulizi ya kushitukiza na wachezaji watakuwa na umakini mkubwa.
Kila timu hapa ni kinara katika Ligi ya nchini kwake, kwa upande wa Bayern Munich wanaongoza katika msimamo wa Ligi nchini Ujerumani, huku ikiwa na alama 56 na Juventus wakiongoza Ligi wakiwa na alama 58 nchini Italia.