NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe, amesema hababaishwi na presha za baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wanaotaka usajili wa wachezaji bora msimu wa 2016/17, kwa madai kuwa wanatumika kuvuruga mipango ya usajili katika klabu hiyo.
Kauli hiyo inatokana na kuvurugika kwa usajili wa mshambuliaji raia wa Burundi, Laudit Mavugo ambaye alitarajiwa kutua Msimbazi hivi karibuni lakini inadaiwa kwamba alimalizana na Simba kwa kusaini mkataba wa miaka miwili kwa dola 20,000 ambazo ni nusu ya fedha walizokubaliana, huku kiasi kingine walitarajia kumalizana akiwa nchini.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Hanspoppe alisema kwamba, bado klabu hiyo ipo katika mchakato wa kuinasa saini ya mshambuliaji huyo licha ya baadhi ya mashabiki kuwa vinara wa kuvuruga mpango huo.
“Suala la Mavugo bado linaendelea na likiwa tayari tutaliweka wazi, hao mashabiki waendelee tu kuwa katika presha kwa maana ndio wavurugaji wakubwa wa mipango yetu ya usajili,” alisema Poppe.
Poppe alisema kwamba, bado klabu hiyo inaendelea na mipango ya kuboresha kikosi cha timu hiyo kwa kusajili wachezaji muhimu ili waweze kufanya vizuri msimu ujao.