30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Hans Pluijm aitega Yanga

PLUIJM

NA MICHAEL MAURUS, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kuwa baada ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa sasa hana uhakika kama anaweza kuendelea kuwapo Jangwani au kusepa.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji tuzo za timu, wachezaji, makocha na waamuzi waliofanya vema msimu uliopita iliyofanyika juzi usiku Hoteli ya Double Tree, Masaki jijini Dar es Salaam, Pluijm alisema anatamani mno kuendelea kuinoa Yanga, lakini hilo litategemea na makubaliano baina yake na viongozi wa klabu hiyo.

“Bado nina uwezo wa kuifundisha Yanga kwa mafanikio makubwa msimu ujao na kutetea ubingwa wetu kwa mara ya tatu mfululizo, kwani nina kikosi cha wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu, uongozi bora na benchi bora la ufundi,” alisema Pluijm.

Alipoulizwa iwapo anaweza kuinoa Yanga kwa muda mrefu zaidi kulingana na umri wake, alisema: “Umri nilionao unaniwezesha kufundisha soka kwa miaka hadi minne ijayo, lakini ninatarajia kusaini miaka miwili tu iwapo tutakubaliana na uongozi.”

Akizungumzia ushiriki wa timu yake Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Pluijm alisema anajivunia umoja na mshikamano uliokuwapo ndani ya klabu hiyo kwa misimu miwili sasa tangu aliporejea Jangwani kwa mara ya pili, ambavyo ndivyo vilivyowawezesha kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

“Ligi ilikuwa ni ngumu sana msimu uliopita, kulikuwa na ushindani mkali, lakini kwa kuwa tulikuwa timu bora, tulifanikiwa kutwaa ubingwa, pongezi kwa kila mmoja aliyehusika katika ubingwa wetu wakiwamo wapinzani wetu,” alisema.

Juu ya tuzo aliyotwaa ya kocha bora wa msimu uliopita, Pluijm alisema: “Tuzo hii imenipa nguvu kubwa ya kufanya vizuri msimu ujao, shukrani kwa wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom Tanzania, TFF, uongozi wa Yanga, wachezaji na wenzangu wa benchi la ufundi.”

Pluijm katika tuzo ya kocha bora, alikuwa akichuana na kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime na Salum Mayanga wa Prisons ya Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles