Na EVANS MAGEGE –Dar es Salaam      |     Â
MWENENDO wa viongozi wa siasa wanaohama kutoka vyama vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo, unaonekana si mchungu tu kwa makada wa siasa za upinzani bali hata wale wa CCM wanakokwenda kujiunga.
Mtazamo huo unajengwa kwa hoja mbalimbali za makada wa pande zote mbili za kisiasa, kwamba wakati wale wa upinzani wakiwatazama wenzao wanaohama kama wasaliti, wale wa CCMÂ wanahisi wanasiasa wanaojiunga na chama hicho wanawazibia uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.
Wakati mwenendo huo wa hamahama ukionekana kudhoofisha na kuchoma upinzani kwa kukosa utetezi katika viti vingi vya udiwani na ubunge, baadhi ya makada ndani ya CCM wamekuwa na manung’uniko ya chini kwa chini dhidi ya utaratibu unaotumiwa na uongozi wa chama chao katika kupitisha majina ya wagombea wanaosimama katika uchaguzi wa marudio wa kujaza nafasi zilizo wazi.
Manung’uniko hayo dhidi ya viongozi wao, yanatokana na kutofurahishwa na kile kinachoitwa ‘uteuzi wa juu kwa juu’ unaoonekana kuwapa kipaumbele wanasiasa waliotoka upinzani kutetea kata au majimbo waliyoyaacha, hatua wanayoiona inawanyima haki yao ya msingi kugombea katika uchaguzi huo wa marudio.
Ikumbukwe kuwa hadi sasa kata 138 na majimbo matano yamefanya uchaguzi wa marudio baada ya viongozi wake waliokuwa upinzani kujiuzulu na kujiunga na CCM.
Katika uchaguzi huo mdogo, CCM iliwasimamisha karibu wanasiasa wote waliohamia kwao kutoka upinzani kugombea nafasi walizoziacha na kushinda tena.
Makada hao wanajenga hisia za kukwazwa na mtindo huo kutokana na kile wanachokiita kwamba waliipigania CCM usiku na mchana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, hivyo ilikuwa ni shauku kwao kuteuliwa katika nafasi za ukuu wa wilaya na nyinginezo.
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA.