Na Shermarx Ngahemera
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Halotel Plc yenye miaka miwili tu nchini, iko njiani kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA).
‘Tunakaribia kwa kishindo,” inasema taarifa ya kampuni hiyo wakati wa kusherehekea miaka miwili ya shughuli zake nchini ikiwa ni kampuni ya tano ya mawasiliano ya simu na inatoka Vietnam ikiwa kampuni tanzu ya Viettel ya jeshi la nchi hiyo.
Kutokana na sheria ya mawasiliano kampuni za simu na migodi mikubwa ya madini zinatakiwa baada ya miaka mitatu kuachia asilimia 25 ya hisa zake kwa kuziuza kwenye soko la hisa la DSE.
Viettel Tanzania Limited au Halotel sasa ni kampuni ya umma ( Plc) na iko mbioni kujiunga na DSE ingawa bado ina mwaka mmoja zaidi kutekeleza hitaji hilo.
Mpaka sasa ni kampuni moja tu ya Vodacom Tanzania Plc ndio imeweza kufanikisha kufikia Agosti 15, mwaka huu na kufanikisha toleo la awali la shilingi bilioni 476 (au dola milioni 213) kutokana na mauzo ya hisa 2,240,000,300 kwa wanahisa zaidi ya 40,000.
Kampuni nyingine tano ziko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na nyingine kukwama kabisa. Toleo hilo lilikuwa la kihistoria kwa ukubwa wa toleo na kiasi cha kila hisa cha shilingi 850.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Plc, Trieu Tanh Binh, anasema kampuni yao ilitoa nuio kwa CMSA na Mamlaka hiyo kuridhia badiliko la jina na masuala mengine yanaendelea baada ya kuainishwa nini cha kufanya kukamilisha usajili huo.
Kampuni nyingine ni Airtel ambayo ilikuwa na tatizo la umiliki ila wameshaelewana na mbia wake ambaye ni Serikali ya Tanzania kila mmoja kuachia asilimia 121/2 na hivyo kuwa na umiliki wa Bharti Airtel kwa asilimia 47.5, Serikali asilimia 271/2 na umma asilimia 25. Dokezo la kuwezesha kuomba kutoa Toleo la Awali (IPO) na nuio la ahadi kwa wanahisa (Prospectus) limeshafanyika na sasa linashughulikiwa na Mamlaka ya Dhamana, Amana na Mitaji ya Tanzania (CMSA) kwa maamuzi rasmi ya kuingia sokoni.
Mkurugenzi Trieu alijinasibu kwa kusema kampuni yake ni mlipaji kodi mzuri na imeshalipa kodi mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 70 toka ianze kazi nchini Oktoba 15, mwaka juzi (2015) na kuwekeza sana kwenye elimu na sekta ya afya ya nchi hii na imeweza kupata wateja zaidi ya milioni tatu na nusu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, makampuni ya simu pamoja na yale ya madini kupitia Sheria ya Fedha (2016) yanatakiwa kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili wananchi wa Tanzania wawe na rujua kwenye makampuni hayo na kufaidi faida zitokanazo katika uchumi wake.
Anasema kuachia simu kampuni inatoa huduma za miamala ya pesa katika kile kinachoitwa huduma ya Halopesa na kudai inaendelea kufanya vizuri kwenye soko.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kuwa Halotel inaongoza kwenye upataji wateja wapya na ina lengo la kuwa namba tatu kwa ukubwa nchini itakapofikia mwisho wa mwaka nyuma ya Vodacom na Tigo kwa kuiangusha Airtel.
Kampuni inaajiri wafanyakazi 1,200 wa moja kwa moja na 20,000 ni watokanao.
Walipoanza kazi Halotel walipata zabuni ya kuunganisha vijiji 3,000 kwenye mtandao wa mawasiliano kwa mara ya kwanza kwa maelekezo ya Universal Communications Services Access Fund (UCSAF) ya Geneva, Uswisi.
Petra yachanganyikiwa
Kampuni ya uchimbaji wa almasi ya Petra inayoendesha mgodi wa Williamson Diamonds ya Mwadui , mkoani Shinyanga iko harijojo kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo ya hisa kama Sheria ya Fedha 2016 inavyodai huku ikiwa na wasiwasi kuhusu kuendelea kuwepo nchini kufuatia serikali kutunga sheria mpya ya madini mwezi Juni 2017.
Mashariti yake sheria hiyo wanaona ngumu kumeza ingawa uzalishaji umeongezeka kwa asilimia sita kufikia Juni mwaka huu kwa kuzalisha karati 225,202 kutoka 212,869 za mwaka jana.
Cha ajabu mapato yamepungua kwa asilimia 26 kwa kupata Dola milioni 58.4 ukifafanisha na Dola milioni 78.9 za mwaka uliotangulia ikidai kwa kukosa almasi bora kwani zimeanguka mapato kufikia Dola milioni 5.2 kutoka dola milioni 25.1 ya mwaka wa fedha uliopita.
Hali tete
Kufuatia mabadiliko makubwa katika Sheria ya Madini Uongozi wa Petra uaona kuwa mambo ni mushikeli kwa Serikali kudai asilimia 16 ya umiliki usiobadilika thamani kama (non-dilutable carryover rights) kwa mgodi ambao Serikali inazo tayari hisa kwa asilimia 25 kuwa ni ngumu kumeza kwani inakuwa na umiliki wa asilimia 41 tayari katika mazingira haya magumu na huko ikitegemea kupata asilimia 50 ya mapato yote ya faida.
Mambo yanakuwa magumu zaidi pale mkataba unapodaiwa ubadilishwe ulingane na ule wa Barrick Corporation ambapo unadai kugawana faida sawa yaani 50 kwa 50.
Isitoshe Serikali ikitaka itachukua asilimia 50 ya mali za mwendesha mgodi ikiwa ni kufidia thamani ya kodi ambayo Serikali ilimpa kupitia misamaha ya kodi.
Hali hiyo imeifanya Petra kutangaza wasiwasi kwa wana hisa wake na kuonesha kuchanganyikiwa kimwenendo.
Wasiwasi huo wa Petra unaonekana kwa wajuzi kuwa hauna msingi na hadaa kwani mgodi unazo takwimu na itifaki nzuri sana za lupanua shughuli.
Kama utafanyika kama ilivyo sasa maisha ya mgodi ni zaidi ya miaka 20 hadi 2033 na uzalishaji unategemewa kuongezeka kutoka karati 225,000 hadi karati 337,500 kwa mwaka kufikia 2019.
Na ukizingatia kuwa Williamson iko kwenye bomba kubwa la almasi la hazina ya karati milioni 39 umri wa mgodi (LOM) au Life of Mine inaweza kuongezwa bila shaka yoyote.
Ripoti ya Petra inaonesha kuwa bado wanaendelea na mazungumzo na Serikali kuhusu kujiorodhesha DSE. Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanaishauri ifanye haraka kwani muda wa subira na kudeka umekwisha na Serikali imeshaamua kuwa asiyependa masharti afunge virago.
Hali imekuwa tete pale kampuni ilipohusishwa na utoroshaji wa almasi ambazo zimekamatwa airport zikidaiwa zilikuwa zinapelekwa nje ya nchi bila vibali rasmi.